Shirikisho la soka duniani FIFA limeanza uchunguzi kuhusu uhamisho wa kiungo kutoka nchini Ureno na klabu ya Manchester United Bruno Fernandes, ambaye uhamisho wake analalamikiwa na klabu ya Sampdoria.
Fernandes alijiunga na Manchester United akitokea Sporting Lisbon, wakati wa dirisha dogo la usajili, kwa ada ya Euro milioni 55, na tayari ameshaifungia klabu hiyo ya Old Trafford mabao matatu na kutoa pasi nne za mwisho kwenye michezo tisa aliyocheza.
Uongozi wa klabu ya Sampdoria uliwasilisha malalamiko FIFA, kwa kushinikiza walipwe asimia 10 ya fedha ya usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, kwa mujibu wa kipengele kilichokua kwenye mkataba wakati wakimuuza mwaka 2017, kuelekea Sporting Lisbon.
Hata hivyo madai hayo yamepingwa vilaki na uongozi wa Sporting Lisbon, kwa kueleza hakuna kipengele chochote kisheria ambacho kinawaamuru kutoa asimilia 10 ya fedha, ambayo inastahili kwenda Sampdoria.
Sporting Lisobon wamewasilisha ushahidi wa mkataba waliosaini na mchezaji huyo, ambao ulivunja makubaliano yake binafsi aliyoingia na klabu ya Sampdoria ambayo yalitoa nafasi ya kulipwa kwa asilimia 10, endapo angeuzwa akitokea nchini kwao Ureno.
Ushahidi huo wa Sporting Lisbon unaonyesha mkataba mpya waliongia na mchezaji huyo ulisainiwa Juni 2018.