Kamati ya Mahusiano ya Kimataifa ya Bunge la Uingereza imetoa taarifa inayo onya juu ya uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia kati ya nchi zenye silaha hizo.
Kamati hiyo imeeleza kwamba kutokana na kushindikana ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi zenye silaha za nyuklia na kadhalika kuendelea kustawishwa kila siku teknolojia na uwezo mpya katika uwanja huo, kumeongeza hatari ya kutokea vita vya silaha za nyuklia dunia.
Mkuu wa Kamati hiyo, David Howell, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuupa umuhimu wasiwasi wa wawakilishi wa bunge hilo na kuongezwa kiwango cha mazungumzo kati ya nchi zenye kumiliki silaha hizo za maangamizi.
Aidha, ripoti ya kamati hiyo juu ya uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia imetolewa ikiwa ni miezi michache imepita baada ya kutolewa ripoti iliyosema kuwa, Marekani na Russia ambazo ni wamiliki wakubwa wa silaha za nyuklia, zimesimamisha makubaliano muhimu ya silaha baina yao.
Mwezi Februari mwaka huu, serikali ya Marekani kwa kisingizio cha kuwa Russia imekiuka mkataba wa makombora kati ya nchi mbili, ilitangaza kwamba imesimamisha Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) kuanzia tarehe 02 Februari na kuanza kutekeleza hatua za kujiondoa kwenye mkataba huo ndani ya miezi sita.
Hata hivyo, kufuatia hatua hiyo, Rais Vladmir Putin wa Russia alisisitiza kuwa hatua hiyo haitakosa jibu na kwamba serikali ya Moscow nayo imesimamisha mkataba huo.