Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anataka makubaliano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya lakini hayuko tayari kuridhia masuala mengine muhimu mawili kwenye mkwamo wa nchi yake na Umoja huo.
Hayo yameelezwa na Waziri anayeshughulikia masuala ya utamaduni kwenye serikali ya Johnson, Oliver Dowden, ambapo amesema kuna uwezakano mkubwa kwa pande hizo mbili kufikia makubaliano kabla ya muda wa mwisho uliowekwa, mwishoni mwa mwezi huu, lakini hana uhakika ikiwa kuna Waziri Mkuu yeyote wa Uingereza atakayekubaliana na masuala mengine yaliyobakia.
Licha ya kutokuyataja moja kwa moja masuala hayo, Uingereza imekuwa na msimamo mkali juu ya mambo ya uvuvi na usimamizi wa masuala ya forodha, baada ya kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya.
Tarehe 31 mwezi huu wa Desemba ndiyo siku ya mwisho kwa Uingereza na Umoja wa Ulaya kukamilisha rasmi hatua ya kujiondowa moja kwa moja kwenye Umoja huo.