Waziri wa Fedha na mipango Dkt. Philip Mpango amefanya mazungumzo na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) ili iweze kuipatia Tanzania mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne toka mkoani Morogoro hadi Jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Dkt. Mpango ametoa ombi hilo Jijini Dodoma wakati alipokutana na Mkurugenzi mtendaji wa bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo Amos Cheptoo anayewakilisha nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema ombi lake kwa Mkurugenzi huyo wa AfDB ni kuona namna gani wanaweza kuanza kuliweka jambo hilo kwenye miradi ambayo benki hiyo imekuwa ikiigharamia ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya njia nne itakayo kuwa na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa njia ya kwenda na ya kurudi.
“Baada ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi tunahitaji usafirishaji kwa njia ya barabara uwe bora na haraka zaidi lakini pia tuweze kupunguza ajali maana kuna ajali nyingi kwa sababu magari yanayokwenda Dar es Salaam na yanayokuja Dodoma au kwenda Mwanza yanapishana kwenye njia moja,” amefafanua Dkt. Mpango.
Akijibu ombi la Waziri Dkt. Mpango Mkurugenzi mtendaji huyo wa Bodi ya wakurugenzi ya benki ya AfDB Amos Cheptoo amesema watahakikisha Tanzania inapata mikopo ya miradi yake ya kimkakati na ya kipaumbele ukiwemo wa ombi hilo la ujenzi wa barabara ya Morogoro hadi Dodoma kwa kiwango kinachokusudiwa.
Kuhusu uwezeshwaji kwa taasisi nyingine nchini Cheptoo amezitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa za mikopo nafuu zilizopo katika benki hiyo kutokana na kuwa na nafasi nzuri ya upatikanaji wake ili ziweze kujikwamua kiuchumi na kutokomeza umasikini barani Afrika.
“Sekta binafsi za Tanzania hazijatumia vizuri dirisha la mikopo ya AfDB ikilinganishwa na chi nyingine za ukanda huu wa Afrika ninakuomba Waziri wa fedha uwahamasishe wakope fedha hizo ili kukuza mitaji yao na kuongeza ajira,” amedisitiza Cheptoo.
Katika hatua nyingine Cheptoo amesema benki ya AfDB ipo katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa msalato jijini Dodoma na tayari benki hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini hapa pamoja na miradi mipya ya kuzalisha nishati ya umeme.
Aidha Mkurugenzi huyo pia amempongeza Rais John Magufuli kwa kuwa kiongozi mwenye maono ambaye amesaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuzitaka nchi nyingine barani Afrika kujifunza kutoka Tanzania.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imefadhili miradi 23 nchini ikiwemo 21 ya umma na miwili ya sekta binafsi ikiwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 2.1 katika nyanja za nishati, miundombinu ya barabara, usafiri, kilimo, maji na usafi wa mazingira.