Serikali kupitia Wizara ya Afya, imeendelea kukamilisha ujenzi wa wodi 45 kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wanaohitaji uangalizi maalum – ICU, katika Hospitali ngazi ya Taifa, Maalum, Kanda na Mkoa kwa kuziwekea vifaa na vifaa tiba ambapo hadi kufikia Machi, 2023 jumla ya ICU 33 zilikuwa zimekamilika na zimeanza kutoa huduma.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema, kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya ICU kutaongeza idadi ya vitanda vya ICU kutoka vitanda 258 vilivyokuwepo na kufikia jumla ya Vitanda 1,000 na kwamba OR-TAMISEMI imekamilisha ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa jumla ya magari 77 yamewasili nchini.
“Hospitali zimeendelea kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ikiwa ni pamoja na huduma ya upandikizaji figo kwa wagonjwa wanne, huduma ya upandikizaji vifaa vya usikivu kwa watoto tisa, huduma ya upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa 11, huduma za upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua na mishipa ya damu kwa wagonjwa 502 na upasuaji wa uti wa mgongo wagonjwa 277,” amesema Ummy.
Aidha ameongeza kuwa, “huduma za upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo maalum “Catheterization Laboratory” kwa wagonjwa 1,069, upasuaji wa mifupa mbalimbali kwa wagonjwa 2,313, kubadilisha nyonga wagonjwa 145, upasuaji wa goti wagonjwa 124.
Nyingine ni upasuaji wa goti kwa kutumia matundu wagonjwa 228, upasuaji wa mfupa wa kiuno wagonjwa 77, upasuaji wa ubongo wagonjwa 160, upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi 364, upasuaji wa dharura 1,679 na upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu kwa wagonjwa 94,” amesema Ummy
Hata hivyo, amesema Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023, jumla ya wagonjwa wa nje ya nchi 812 wamehudumiwa na Hospitali za Taifa, Maalum na Kanda ukilinganisha na wagonjwa 368 kipindi kama hiki mwaka 2021/22.
Ameongezea kuwa kusema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo na kuanzisha nyingine kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba katika nchi za Afrika.