Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wakuu wa majimbo 16 nchini humo wamekubaliana kuongeza makali ya amri ya kuvaa barakoa pamoja na kufungwa mapema maduka ya kuuza pombe katika maeneo yenye visa vingi vya COVID-19.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano uliofanyika Oktoba 14, saa chache tangu Ujerumani kuripoti maambukizi mapya 5,000 ya virusi vya Corona, katika kipindi cha saa 24, kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kushuhudiwa tangu katikati ya mwezi Aprili.
Mapendekezo yaliyotolewa yanataka amri ya kuvaa barakoa ambayo tayari ni lazima ndani ya vyombo vya usafiri na maduka nchini Ujerumani, pia itekelezwe kwenye maeneo ya umma yaliyo na msongamano katika wilaya zenye maambukizi makubwa ya COVID-19.
Wakati hali nchini Ujerumani bado inatia moyo ikilinganishwa na mataifa mengine barani Ulaya, Kansela Merkel amesema ni muhimu kupunguza kiwango cha maambukizi.
Wakati hayo yakijiri nchini Ujerumani, taifa jirani la Ufaransa limetangaza kuwa siku ya Jumamosi litaanza kutekeleza marufuku ya kutoka nje usiku kwenye mji mkuu Paris, na miji mingine 8 mikubwa katika juhudi zake za kukabiliana na janga la virusi vya Corona.