Mkutano wa pili wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji, unatarajia kuwakutanisha jumla ya Washiriki 900 toka Mataifa mbalimbali ya nchi za Umoja wa Afrika, Oktoba 9 – 11, 2023 Jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania itakuwa na washiriki 200.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Doroth Gwajima amesema washiriki hao 200 watatoka katika Mikoa mbalimbali, hasa ile yenye takwimu za juu za ukeketaji, kwani wao wana uzoefu wa utekelezaji wa afua za kutokomeza vitendo hivyo.
Amesema, “kwa mujibu wa takwimu za Afya, Idadi Watu na Viashiria vya Malaria za mwaka 2015/16 zinaonyesha kwamba ukeketaji umepungua kutoka asilimia 30 mwaka 2010 hadi asilimia 10 mwaka 2015 na kuna baadhi ya Mikoa takwimu zake ni za juu zaidi ya wastani.”
Ameitaja Mikoa hiyo kuwa ni Manyara asilimia 58, Dodoma asilimia 4, Arusha asilimia 41, Mara asilimia 32, Singida asilimia 31 na Tanga asilimia 14 na kwamba wanalenda kutoa fursa kwa wadau wanaopambana na ukeketaji, kuunganisha nguvu za pamoja, kubadilisha uzoefu, kujengeana uelewa na maarifa, ili kuimarisha mapambano ya kutokomeza ukeketaji Afrika.