Mamlaka ya Mapato nchini Kenya – KRA, imeanza kuwatumia Mawakala wake ambao wamefuzu mafunzo kupita kila kaya na kwa Wafanyabiashara, ili kuthibitisha wanazingatia ulipaji ushuru ili kuongeza mapato ya serikali.
Mawakala hao wapatao 1,400 ambao ni Maafisa waliohitimu mafunzo katika Shule ya Kuajiri Wanajeshi huko Eldoret mwezi uliopita, watapita maeneo hayo kuhakikisha ulipaji ushuru unazingatiwa, ili kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, Maafisa hao pia watawezesha usajili wa Biashara Mtandaoni na kuwasaidia walipa ushuru kuthibitisha kodi anayotakiwa kulipa na kuweza kuwatambua Wafanyabiashara wanaokwepa kodi, ikiwemo kuthibitisha maelezo ya walipa ushuru pamoja na kuhakikisha kanuni za mifumo ya ulipiaji kodi na ukusanyaji wa data za walipa ushuru zinasaidia mifumo ya ndani.
Utaratibu huo, unatajwa kama sehemu ya mpango wa serikali ya Rais William Ruto ya kuongeza mapato zaidi ya jumla ya shilingi trilioni 2.9 kugharamia bajeti yake ya shilingi trilioni 3.67, kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.