Rais wa heshima wa FC Bayern Munich, Uli Hoeness ana imani Mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane atajiunga na miamba hiyo ya soka ya Ujerumani wakati huu wa majira ya kiangazi.
Klabu hizo mbili zilikutana Alhamisi (Julai 13) kujadili uwezekano wa nahodha huyo wa timu ya taifa ya England kujiunga na Bayer ingawa hakuna hatua ya maana iliyofikiwa katika kikao hicho kilichomhusisha mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy na Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern, Jan-Christian Dreesen.
Mazungumzo bado yako wazi, na Bayern wana imani watafanikiwa katika adhima yao ya kumsajili mfumania nyavu huyo wa timu ya Taifa ya England.
“Harry Kane ameweka wazi kwenye mazungumzo yake yote juu ya uamuzi wake na kama atasimamia kauli zake, basi tutampata kwa sababu Tottenham wataharakisha kumuuza,” alisema Hoeness.
“Kane anataka kucheza Ligi ya Mabingwa na bahati kwetu Tottenham haipo kwenye mashindano haya msimu ujao.”
Kwa upande wao Tottenham wataendelea kujaribu kumshawishi Kane kusaini mkataba mnono, lakini hofu yao anaweza kujiunga na wapinzani wao Ligi Kuu ya England kama watamuacha amalize mkataba wake.
Kane hajaondoa uwezekano wa kuangalia nafasi yoyote katika hatua hii na alikuwa sehemu ya kikosi cha Tottenham kilichoenda Australia kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Ilifahamika mapema juma lililopita kuwa Tottenham na Bayern walifanya mazungumzo kuhusu uhamisho wa Kane, ambaye alikutana na kocha mpya wa timu hiyo Ange Postecoglou.
Postecoglou aliweka Kane ni sehemu ya mipango yake ya kuijenga upya Tottenham, hivyo angependa kuendelea kuwa nae.