Serikali nchini, imesema baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG, kutolewa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kufanyia kazi maelekezo ya Rais ya kufanya uchunguzi kwenye maeneo yote ambayo yametolea taarifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari maelezo, Gerson Msigwa amesema sambamba na hatua hiyo pia Serikali inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema, “ripoti hii inahusisha rasilimali za umma, nawahakikishia kuwa hakuna kitu kitakachoachwa, Pale ambapo kuna taasisi imehusika katika upotevu wa mali za umma hatua zitachukuliwa.”
“Ripoti ya CAG ni moja ya nyenzo ambazo Serikali inazitumia katika kusimamia rasilimali za Watanzania, pia inatumika katika kuangalia ni maeneo gani yanahitaji kuongezewa nguvu katika usimamizi wa rasilimali za Watanzania na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa ili rasilimali hizo ziendelee kuwa salama”. Amesema Msigwa
Ameongeza kuwa, mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya kwanza km 1,219 inayotoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na awamu ya pili KM 1,505 itakayofika mpaka Kigoma inaendelea, kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kimefikia 98.2%, kipande cha Morogoro hadi Makutupora kimefikia 93.3%, kipande cha Makutupora hadi Tabora kimefikia zaidi ya 2% na kipande cha Mwanza hadi Isaka kazi inaendelea.
Msigwa ameongeza kuwa, “ripoti ya CAG imetolewa lakini haizuii kazi za Serikali kuendelea hasa katika miradi yetu ya kimkakati, tuliagiza mabehewa 59, tayari mabehewa 14 yalishakuja, mabehewa 45 maandalizi yake yamekamilika kwa 93% hivyo wakati wowote yatafika nchini.”
“Tunanunua vichwa vya treni 17 pamoja na treni zenye vichwa mbele na nyuma maarufu kama treni mchongoko, mpaka sasa maandalizi ya ununuzi wa vichwa 17 imefikia 45% na treni mchongoko maandalizi yamefikia 38.1%”. Amesema Msigwa.
Hata hivyo, amesema Kazi ya kutengeneza na kuyaandaa mabehewa 1,430 yaliyoagizwa kutoka Nchini China inaendelea, kazi hiyo imefikia 40%. Kazi ya mabehewa 30 na vichwa viwili ambavyo vimenunuliwa Nchini Ujerumani inaendela na yatakapokamilika yataletwa Nchini Tanzania.