Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uledi Abbas Mussa amesema mamlaka hiyo imekuwa ikionesha ufanisi katika makusanyo ya kodi na kwamba ulipaji wa kodi bila shurti ni kuonesha uzalendo hivyo hawatatumia nguvu kutekeleza majukumu yao.
Mussa ameyasema hayo wakati wa kikao kazi baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wahariri wa vyombo vya habari nchini na kuongeza kuwa walipa kodi wanatakiwa kuwa huru na wale wenye changamoto wajitokeze ili kukaa meza moja kujadili na kupata muafaka.
Amesema, “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alituelekeza kwamba tujenge utamaduni wa kukusanya mapato ya Serikali bila kutumia mabavu na ndio maana tunawaelekeza maafisa wetu kukusanya mapato bila kutumia nguvu.”
Musa ameongeza kuwa, “Haiwezekani hata siku moja, mmewashawahi kukuta mfugaji anamchinja kuku aliyeatamia au anayetaga mayai hata kama ni sikukuu yuko radhi akanunue mbuzi mwingine au kuku mwingine siyo anayetaga. na hili tunalifanya kwa walipa kodi wetu wanaendelea kufanya biashara zao ili wawe walipa kodi wazalendo na waaminifu.”