Serikali imesema kuwa tatizo la maradhi yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya akili yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku huku vyanzo vyake vikiwa ni pamoja na urithi, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, matatizo ya kisaikolojia pamoja na hali ngumu ya maisha.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, alipokuwa akizindua Bodi ya Hospitali ya Mirembe Mkoani Dodoma.
Akiongea mbele ya Watendaji wa Bodi hiyo, wageni waalikwa pamoja na Viongozi wa hospitalini hapo, Waziri Ummy amesema kuwa, kundi lililoathirika Zaidi na kadhia hiyo ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
“Matatizo haya yamekuwa yakisababisha vifo milioni 3.3 kila mwaka Duniani kote, hata hivyo taarifa ya Wizara yangu inaonyesha kwamba idadi ya watu wanaougua magonjwa ya akili inaongezeka kwa kasi kubwa kutoka wagonjwa 136,710 mwaka 2011/2012 hado wagonjwa 448,997 mwaka 2015/2016”, amesema Ummy.
Aidha, ameongeza kuwa takwimu za hospitali ya Mirembe zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, jumla ya wagonjwa Zaidi ya 60,000 wenye magonjwa ya akili na waathirika wa dawa za kulevya walipatiwa huduma za afya na utengamao.
Hata hivyo, Ummy amesema kuwa kwa kutambua majukumu makubwa ya hospitali hiyo na kutatua changamoto zinazohusiana na magonjwa hayo, Serikali imeamua kuunda Bodi ya hospitalini hapo lengo likiwa ni kutekeleza dhana ya Utawala Bora na Utoaji wa Huduma Bora za Afya ya Akili kwa mujibu wa mapango mkakati na sera za nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Gadi Kilonzo amempongeza Waziri Ummy na kwa kuzindua bodi hiyo na amemuhakikishia kuwa bodi hiyo itatekeleza maagizo yote pamoja na majukumu iliyopewa ili kuboresha utendaji kazi hospitakini hapo.
Wajumbe waliochaguliwa kuunda bodi hiyo ni Profesa Gadi Kilonzo ambaye ndio Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Erasmus Mndeme ambaye ni Katibu wa Bodi na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mirembe, Dkt. Mpona Boniventura ambaye ni Mwakilishi kutoka chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Joseph Mbatia, Ndugu John Sipendi, Ndugu Ernest Kabohola, Ndugu Jane Magembe pamoja na Ndugu Clavery Lyela