Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania umeongezeka kwa kiasi kidogo ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki.

Takwimu hizo zimetajwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC), Ephraim Kwesigabo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Januari mwaka 2017.

Kwesigabo amesema kuwa nchi zote za Afrika Mashariki hali ya mfumuko wa bei huwa unafanana na kwa kawaida Tanzania inajilinganisha na nchi za awali za Kenya na Uganda kwa sababu nchi zingine zina tofauti kidogo katika utoaji wa takwimu zao.

“Takwimu zilizoishia mwezi Disemba mwaka 2016, zinaonyesha kuwa nchi ya Uganda mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 5.7 hadi asilimia 5.9 na nchini Kenya umeongezeka kutoka 6.35 asilimia  hadi asilimia 6.99 hivyo kwa ujumla mfumuko wa bei Tanzania ni mdogo,”amesema  Kwesigabo.

Aidha, ameongeza kuwa, farihisi za bei zimeongezeka kutoka 100.71 mwezi Januari, 2016 hadi 105.92 mwezi Januari, 2017 wakati mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Januari,2017 zimeongezeka hadi asilimia 7.6 kutoka asilimia 7.0 ilivyokuwa mwezi Disemba, 2016.

Hata hivyo amesema takwimu za mwezi kwenye upande wa mfumuko wa bei  za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula, Mkurugenzi amefafanua kuwa bei za vyakula nyumbani na migahawani zimeongezeka kutoka asilimia 7.4 mwezi Disemba 2016 hadi kufikia asilimia 8.2 kwa mwezi Januari 2017.

Mfumuko wa bei nchini kwa kipimo cha mwaka umeongezeka hadi asilimia 5.2 wakati mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi Januari, 2017 umeongezeka kwa asilimia 0.8.

Wazazi wapewa onyo kuhusu mchezo wa kamari kwa watoto
Ummy Mwalimu azindua bodi mpya Hospitali ya Mirembe