Umoja wa Ulaya umesema kuwa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May hakutobadili chochote kwenye msimamo wake kuelekea makubaliano yaliyofikiwa kuiwezesha Uingereza kujiondoa kutoka Umoja huo.
Msemaji wa rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker amesema kuwa ameupokea uamuzi wa May kwa masikitiko makubwa na kuongeza kuwa baraza la viongozi wa Umoja wa Ulaya lilikwishaweka msimamo wake kuhusu makubaliano ya Brexit.
Aidha, May alitangaza kujiuzulu wadhifa wa waziri mkuu baada ya kushindwa kuwashawishi wabunge kuunga mkono mpango wake wa kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, Brexit.
Kiongozi wa ujumbe wa majadiliano ya Brexit wa Umoja wa Ulaya, Michel Barnier, aliandika kwenye ukarasa wake wa Twitter akiusifu msimamo wa Theresa May kama waziri mkuu kwa kufanya kazi kuwezesha Uingereza kuondoka salama kutoka Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wamemsifu May kwa kazi kubwa na ya kujitolea aliyoifanya kujaribu kukamilisha mchakato wa Brexit kwa maslahi ya nchi yake.