Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anafanya kile alichokiita kuwa ni mawasiliano ya mfululizo na Urusi, Ukraine, Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya katika jaribio la kurejesha uuzaji wa nafaka ya Ukraine wakati mgogoro wa chakula duniani ukizidi kuwa mbaya zaidi.
Guterres ameonya kuwa Vita vya Urusi nchini Ukraine vimesababisha bei za kimataifa za nafaka, mafuta ya kupika, nishati na mbolea kupanda, amesema hiyo itafanya mizozo ya chakula, nishati na kiuchumi katika nchi maskini kuwa mbaya zaidi.
Akiuhutubia mkutano wa ngazi ya mawaziri kuhusu chakula ulioandaliwa mjini New York, Guterres ameiomba Urusi kuruhusu usafirishaji salama wa nafaka iliyohifadhiwa katika bandari za Ukraine na chakula cha Urusi na mbolea kufikishwa kikamilifu na bila vizuizi kwa masoko ya ulimwengu.
“Mgogoro wa chakula hauheshimu mipaka, na hakuna nchi inayoweza kuutatua peke yake. Fursa yetu pekee ya kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye njaa ni kuchukua hatua pamoja, haraka na kwa mshikamano.” Amesema.
Guterres ambaye alizuru Moscow na Kyiv mwezi uliopita, amesema ana matumaini ya kupatikana suluhu lakini safari bado ni ndefu.
Ameongeza kuwa madhara makubwa ya kiusalama, kiuchumi na kifedha yanahitaji nia njema kutoka kila upande ili kutatuliwa.