Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya afya na huduma, wanapata malipo ya chini zaidi kuliko sekta nyingine za kiuchumi na wanalipwa asilimia 24 pungufu ya wenzao wa kiume hata pale wanapokuwa na vigezo sawa katika soko la ajira.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya uchambuzi Duniani, kuhusu ukosefu wa usawa wa kijinsia kwenye mishahara katika sekta ya afya uliofanywa na mashirika mawili ya umoja wa Mataifa ya ajira duniani ILO na afya WHO na kusomwa jijini New York Marekani katika mkutano wa ngazi za juu unaofanyika katika Makao Makuu ya UN.
Ripoti hiyo, imesema pengo ghafi kati ya wanawake na wanaume ni asilimia ishirini lakini likiangaziwa kwa undani zaidi kwenye masuala ya elimu, umri na muda wa kufanya kazi linaongezeka na kufikia asilimia 24 na hivyo kufanya wanawake kulipwa kiwango cha chini zaidi kwenye soko la ajira ikilinganishwa na wanaume.
Hata hivyo inarifiwa kuwa Wanawake wanashikilia asilimia 67 ya nguvu kazi katika sekta ya afya, ambapo ripoti pia imegundua mishahara katika sekta ya afya ipo chini ikilinganishwa na sekta nyingine za kiuchumi.
Mkurugenzi wa kitengo cha nguvu kazi wa WHO, Jim Campbell amesema ushahidi na uchambuzi uliomo kwenye ripoti hiyo lazima utumike kuzijulisha Serikali, waajiri na wafanyabiashara kuchukua hatua madhubuti kuleta usawa wa kijinsia kwenye malipo.
“Na zilipotafutwa sabababu zinazofanya wanawake kulipwa kidogo kuliko wanaume walio na sifa sawa za soko la ajira katika sekta ya afya na huduma kote ulimwenguni kwa kiasi kikubwa ripoti hii inaonesha kuwa bado hakuna majibu sahihi,” amesema Campbell.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya masharti ya kazi na usawa wa ILO, Manuel Tomei amesema anatumai ripoti hiyo itasaidia kuchochea mazungumzo na hatua zinazohitajika kuleta usawa, na kudai kuwa wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti za kisera ikijumuisha mazungumzo muhimu ya kitaasisi.
“Hakutakuwa na ahueni jumuishi, dhabiti na endelevu bila sekta ya afya na huduma imara na hatuwezi kuwa na huduma bora za afya na uangalizi bila mazingira bora na ya haki ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na mishahara ya haki kwa wafanyakazi wa afya na huduma, ambao wengi wao ni wanawake,” amefafanua Tomei.
Hata hivyo, ripoti hiyo imekumbusha namna janga la COVID-19 lilivyoionesha dunia umuhimu wa sekta ya afya na wafanyakazi wake, na kusema huduma hiyo imestahimili malipo duni kwa ujumla na mapungufu makubwa ya mishahara ya kijinsia na mazingira magumu kwa kipindi kirefu.