Wataalamu huru wa haki za binadamu, walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi za kuzuia na kuadhibu vitendo vya ukeketaji wa wanawake nchini Sierra Leone na kwingineko Barani Afrika.
Hatua hiyo, inafuatia kesi ya jinai juu ya kifo cha mwanafunzi mwenye umri wa miaka 21 aliyefanyiwa vitendo hivyo vya kikatili katika wilaya ya Bonthe, nchini Sierra Leone ambapo wataalam hao watatu wametoa tamko la kulaani ukeketaji wakiuita kuwa ni “aina mbaya zaidi ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na ni mateso”.
Wamesema, ukeketaji unakiuka haki za msingi za waathriwa wake, ikiwa ni pamoja na hadhi yao ya kimwili na haki za kutoteswa au kutendewa vitendo vingine vya kikatili na haki ya maisha, afya ya ngono na uzazi na kwamba ukeketaji ni desturi za kibaguzi na zimejikita katika kanuni za kijamii na uchu wa mamlaka.
“Kama desturi zingine za asili zenye madhara za asili kama hiyo, ukeketaji unaonyesha na kuendeleza mwelekeo mpana wa ukosefu wa usawa wa kijinsia na tunasisitiza kuwa ukeketaji hauwezi kurekebishwa au kutumiwa kama uhalali wa kutumia mila za kitamaduni na kidini kwa kuhatarisha ustawi wa wanawake na wasichana.”
Aidha, wameongeza kuwa, “Lazima mila hizo zifafanuliwe kulingana na mwelekeo mpana wa unyanyasaji wa kijinsia, ambao hauwezi kuendelea bila kuadhibiwa maana ripoti zinaonesha kesi ya jinai dhidi ya mmoja wa wahalifu wanaoshtakiwa kwa ukeketaji uliosababisha kifo cha mwathiriwa imezuiliwa.
Hata hivyo wameongeza kuwa, “Kukosekana kwa sheria inayojitolea na inayotekelezeka ambayo inaharamisha na kuadhibu kwa uwazi ukeketaji kunazuia uchunguzi wa Mahakama.
Sambamba na hilo, pia uchunguzi mwingine ni kuhusu watu kuteswa na vitendo hivi hatari na mauaji haramu, ila sheria na sera zinahitaji kutoa mifumo ya wazi ya uwajibikaji na vikwazo vya kinidhamu kuhusiana na ukeketaji.”
Hata hivyo, wameitaka Serikali ya Sierra Leone na zile za nchi mbalimbali barani Afrika, kuanzisha vifungu maalum vya kisheria vinavyokataza vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha mkataba wa maelewano na watendaji wa ndani na kurekebisha sheria ya haki za mtoto ili kupiga marufuku ufanyaji wa tohara kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18.