Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya afya ulimwenguni WHO, na la Kuhudumia Watoto UNICEF, wametangaza kuongeza nguvu kwenye juhudi za kuzuia kuenea kwa Ugonjwa wa kipindupindu nchini Malawi, kufuatia vifo vya watu 58 vilivyorekodiwa ambavyo ni sawa na asilimia 3.9.

Taarifa ya mashirika hayo iliyotolewa mjini Lilongwe, Malawi imesema mlipuko huo ambao hapo awali ulianzia kusini mwa nchi hiyo, sasa umeenea katika mikoa ya kaskazini na katikati ya Malawi.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyolewa kwa vyombo vya habari jumatatu ya tarehe 22 Agosti 2022 mpaka siku hiyo wagonjwa wenye kipindupindu walikuwa ni 1,483 ambapo WHO na UNICEF wamesema kila kifo kitokanacho na Kipindupindu kinaweza kuzuilika.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Malawi, Rudolf Schwenk amesema, “Athari za mlipuko mkubwa zaidi zitalemea sekta za huduma za afya ya umma ambazo tayari zimeelemewa na mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini humu, hivyo ni lazima kuchukua hatua sasa” huku akiongeza kuwa “Habari njema ni kwamba tunajua suluhisho.”

Mhudumu wa Afya wa WHO, akikagua masanduku ya dawa za matibabu mbalimbali. Picha na Nyasa Times.

Licha ya juhudi zinazoendelea katika kukabiliana na mlipuko wa kitaifa wa kipindupindu, mapungufu makubwa yameonekana katika hitaji la haraka la kugunduliwa na kudhibiti mapema, kupatikana kwa vifaa muhimu vya kusimamia wagonjwa na matibabu ya maji, usafi wa kibinafsi na uhifadhi wa maji katika ngazi ya kaya na kutoa elimu kuhusu usafi.

Mwakilishi wa WHO nchini Malawi, Neema Rusibamayila Kimambo amesisitiza kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wizara ya Afya ya Malawi katika kutekeleza udhibiti wa haraka na wa muda mrefu wa kipindupindu.

Tangu kutangazwa kuzuka kwa mlipuko wa kipindupindu mwezi Machi 2022, UNICEF na WHO wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya, Maji na Usafi wa Mazingira, mamlaka za wilaya, na wengine, katika kuandaa na kuratibu mpango wa kukabiliana na kuwasilisha vifaa na huduma muhimu kwa familia na jamii katika wilaya zilizoathiriwa na kipindupindu nchini Malawi.

UN yataka Mataifa kuchukua hatua kali kwa wakeketaji
Maandamano kupinga gharama za Maisha yashika kasi