Kituo cha afya cha Dabalo mkoani Dodoma kimepokea msaada wa vifaa tiba pamoja na majengo katika kuendelea kukabiliana na huduma za dharura za Afya ya mama na mtoto.
Msaada huo wenye gharama ya Shilingi 615,205,539 umetolewa na shirika la Kimataifa la UNFPA kwa msaada wa Denmark kupitia mradi wa RMNCH wa Serikali ya Tanzania na umepokelewa na Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Angelah Kairuki.
Kairuki amesema pamoja na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, Vifo vya uzazi na watoto wachanga vimesalia kuwa juu Nchini kwa muongo uliopita, ambayo ni zaidi ya vifo 500 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai.
“Hivi majuzi, takwimu (TDHS-MIS 2022) zimeonyesha kuwa vifo vinavyotokea katika mwezi wa kwanza wa maisha vinachangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vya watoto wachanga. Ukweli wa kusikitisha ni kwamba vifo hivi vingi vinaweza kuzuilika ikiwa sote tutachukua hatua madhubuti!.” Amesema Waziri Kairuki.
Amesema miongoni mwa vipaumbele vya juu vya Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na Uhamasishaji na Utoaji wa Huduma bora za Afya karibu zaidi na wananchi, na kwa gharama ambazo wanaweza kuzimudu.
Ameongeza kuwa, “Ili kukabiliana na changamoto hizi kunahitajika juhudi za pamoja kati ya serikali na Wadau wengine wa Maendeleo katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingine Mtambuka.”
Waziri Kairuki ameongeza kuwa miongoni mwa vipaumbele vya juu vya Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na Uhamasishaji na Utoaji wa Huduma bora za Afya karibu zaidi na wananchi, na kwa gharama ambazo wanaweza kuzimudu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA nchini Tanzania Mark Bryan Schreiner, amesema kupitia mradi huo uliodhaminiwa na Denmark, Kituo cha afya cha Dabalo kimefaidika kwa mambo makubwa Mawili ambayo ni ukarabati wa wodi ya wazazi na chumba cha upasuaji pamoja na vifaa tiba na gari la kusafirisha wagonjwa wa dharura.
“Kupitia uchangiaji huu wa huduma za uzazi Msaada wa Denmark umesaidia kubadilisha maisha ya mamilioni ya wanawake, vijana na watoto” amesema Schreiner.
Naye Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Nørgaard Dissing-Spandet amesema huduma za Afya msingi ndio uti wa mgongo wa mfumo mzima wa afya katika nchi yoyote, na kwa kuzingatia hilo ubalozi wa Denmark umeendelea kushirikiana na UNFPA kutoa msaada katika fungu la Afya kwa miongo miwili.
“Kubeba mimba ni hatari ndio maana nchini Tanzania vifo vitokanavyo na uzazi ni 21% ya vifo vya wanawake na [TDHS2016]. Kwa hali hii ubalozi wa Denmark unayo furaha kuimarisha huduma za afya na kuongeza ufanisi katika kufikia huduma za afya ya uzazi kwa kuwa ni muhimu nchini Tanzania.” Amesema Bi Mette.
Bi Mette ameonyesha furaha yake kwa kuona vifaa tiba na Majengo ya huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga yanakabidhiwa katika kituo cha afya cha Dabalo.
UNFPA imekuwa ukiendelea kusaidiana na serikali ya Tanzania katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na kuendelea muleta matokeo chanya nia ikiwa ni kufikia asilimia sifuri ya vifo vya vya wajawazito na watoto.