Kutokuwa na uhakika wa chakula duniani kote, janga la mabadiliko ya tabia nchi, vita nchini Ukraine na dharura nyinginezo zinazotawala kuanzia Barani Afrika na nchi ya Afghanistan ni kati ya sababu kubwa zilizowafanya watu milioni 100 wa maeneo hayo kuyakimbia makazi yao.
Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi ameyasema hayo hii leo Juni 17, 2022 na kuongeza kuwa kila mwaka katika muongo uliopita, idadi ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao imekuwa ikiongezeka.
“Jumuiya ya Kimataifa italazimika kushikamana ili kuchukua hatua kushughulikia janga hili la kibinadamu, kutatua migogoro na kusaka suluhu za kudumu, la sivyo hali hii mbaya itaendelea,” amesema Grandi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kila mwaka ya mwelekeo wa Kimataifa wa watu wanaotawanywa inasema mtu mmoja kati ya watu 78 duniani anaonekana kuhama eneo analoishi na kufanya mabadiliko makubwa ambayo ni wachache wangeyatarajia kuyaona kwa muongo mmoja uliopita.
Ripoti hiyo inasema kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, idadi ya waliokimbia makazi yao kutokana na vita, ghasia, mateso na ukiukwaji wa haki za binadamu ilifikia watu milioni 89.3.
“Hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia nane kutoka mwaka 2020 na ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya miaka 10 iliyopita”, wamesema waandishi wa ripoti hiyo wakihusisha ongezeko la mwaka jana na migogoro mingi inayoongezeka na mipya iliyozuka.
UNHCR inasema idadi ya watu milioni 100 waliokimbia makazi yao ilifikiwa mwezi Mei mwaka huu, ikiwa ni wiki 10 tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kusababisha uhaba mkubwa wa nafaka na mbolea duniani.
Kuhusu mgogoro wa kutokuwa na uhakika wa chakula Duniani unaoendelea hivi sasa una namna ambavyo unaweza sababisha watu wengi zaidi kuyakimbia makazi yao, Kamishna Mkuu Grandi amesema hawezi kufikiria ni kwa jinsi gani inaweza kuwa vinginevyo.
“Endapo unakuwa na mgogoro wa chakula kuongezea na changamoto zingine za vita, ukiukwaji wa haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi, vitaongeza tu mwelekeo ulioelezewa katika ripoti hii na ambao tumeshuhudia ukiongezeka tayari katika miezi michache ya kwanza ya mwaka huu.”
UNHCR inasema miongoni mwa majanga mapya makubwa ya kibinadamu yaliyoangaziwa mwaka 2021, vipo vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia iliyosababisha takriban watu milioni 2.5 kuyahama makazi yao, huku wengine milioni 1.5 kati yao wakirejea makwao kwa mwaka huo.