Licha ya Serikali kuongeza kasi katika utoaji wa elimu kwa jamii, bado watu wanaoishi na virusi vya ukimwi mkoani Njombe wamekiri kuendelea kukabiliwa na vitendo vya unyanyapaa katika mihadhara na matukio ya kijamii ikiwemo misiba.
Wamesema Baadhi ya vitendo vya unyanyapaa ambavyo vimekithiri ni pamoja na lugha chafu kwamba watu hao wanatumia mashudu , kutengwa kwenye baadhi ya mambo ya kijamii pamoja na kusemwa vibaya nyakati za mazishi yao jambo ambalo linawafanya kujihisi wapweke na wadhaifu.
Wameeleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi mkoani Njombe ambayo Kimkoa yalifanyika Desemba mosi 2019 katika kijiji na Kata ya Ilembula wilayani Wanging’ombe.
Baadhi ya mashuhuda wanaoishi na VVU akiwemo Bi, Selafia Nyika na Bw, Jeremia Mtovisala wamesema kwamba wamekuwa wakikumbwa na vitendo vingi vya unyanyapaa hatua ambayo inawafanya kujiona kama hawana haki ya kuishi na Jamii.
Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Comrade Ally Kassinge aliye muwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka.
Takwimu za maambukizi kwa mkoa wa Njombe bado zimeendelea kuwa juu licha ya kushuka kutoka asilimia 14.8 hadi asilimia 11.4 hatua inayofanya Serikali kuongeza kasi ya kutoa elimu na mapambano dhidi ya ukimwi ili kufikia sifuri tatu ifikapo 2030 katika halmashauri zote za Mkoa huo ambao ni kinara kwa maambukizi Nchini.
Katika maadhimisho hayo Serikali imetangaza mpango mkakati mpya wa miaka mitano wa kuanzia 2019 hadi 2023 utakaosaidia kupunguza maambukuzi mapya, kutoa hamasa ya kupata tohara, kuanza dawa na wanaume kujitokeza kupima kwakuwa ni kundi ambalo limetajwa kususia kupima VVU.
Simon Mdende Mratibu wa mpango huo na kaimu mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt Manyanja Mponeja wameeleza hayo sambamba na kutoa Wito kwa Jamii.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa Mwaka 2019 inaeleza kuwa “Jamii ni chachu ya mabadiliko iungane kupinga maambukizi”.