Kocha Mkuu wa Namungo Denis Kitambi ameendelea kukinoa kikosi chake kwa ajili ya mechi mbili za mwisho za kumaliza msimu lakini taarifa za ndani ya timu hiyo zinaeleza kocha huyo yupo kwenye mtego wa kuachwa.
Kitambi alijiunga na Namungo katikati ya msimu huu akichukua nafasi ya Mzambia Honor Janza, licha ya kuifanya timu kuwa katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi lakini kuna baadhi ya viongozi wanaamini anatakiwa kuwapisha na kushusha mtaalamu mpya.
Kiongozi mmoja wa Namungo amesema huenda mwisho wa msimu huu, wauaji hao wa kusini wakaachana na Kitambi kutokana na kile kinachoelezwa timu kutocheza vizuri na kufikia malengo ambayo ilikuwa ni kumaliza katika nafasi nne za juu.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa tayari timu hiyo imeanza kutafuta kocha mpya ambaye ataanza msimu na timu baada ya kuachwa kwa Kitambi na miongoni mwa makocha wanaopigiwa chapuo kutua kwa Wanakusini hao ni Fred Felix ‘Minziro’ kutoka Geita Gold, anayewindwa pia na Mbeya City.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omary Kaya amepinga jambo hilo na kusema; “Kwa sasa tunafanya maandalizi ya mechi zilizobaki ili tumalize msimu salama, hizo habari za kuachana na kocha sizijui na tunasubiri msimu uishe.”