Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema serikali inalipa pensheni kwa wastaafu kwa wakati kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi.

Katambi ameyasema hayo hii leo Mei 26, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodemus Maganga ambaye ametaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pesheni za wastaafu zinalipwa kwa wakati.

Amesema katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa pensheni zao kwa wakati, Serikali kupitia mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF imeweka utaratibu mahsusi wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki kupitia kwenye akaunti zao za Benki kabla au ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi.

Aidha, ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2023 idadi ya wastaafu wanaolipwa pensheni katika Mifuko ya PSSSF na NSSF imefikia 186,605 (ikijumuisha PSSSF wastaafu 158,735 na NSSF wastaafu 27,870).

Hata hivyo, Katambi amesema mifuko inaendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya ulipaji wa mafao ili kuhakikisha maombi ya wastaafu wapya yanafanyiwa kazi kwa haraka na kuanza kulipwa pensheni ndani ya kipindi kisichozidi siku 60 kama Sheria inavyotaka.

Uongozi Namungo wapishana kauli ishu ya kocha mpya
Chalamila, Mwasa wakabidhiana ofisi Kagera