Baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya alizeti jijini Dar es Salaam wamelazimika kufunga shughuli zao kutokana na kukosa malighafi, huku bei ya mafuta hayo ikipaa kipindi cha msimu wa sikukuu.
Wakizungumza na gazati la Nipashe, baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti vilivyopo katika Sokola Sido jijini hapa, wamesema mwaka huu umekuwa tofauti na miaka mingine kutokana na malighafi kuisha mapema zaidi.
Mmoja wa wamiliki hao, Charles Mwakitalima, amesema uhaba wa malighafi hiyo umetokana na mvua zilizonyesha kupita kiasi katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambazo ziliharibu alizeti mashambani.
Amesema wakulima walijitahidi kulima kwa wingi zao hilo, lakini baada ya mvua kuzidi ziliharibu na kusababisha kuozazikiwa bado ndogo shambani, huku baadhi zikioza baada ya kukomaa wakati mvua ikiendelea kunyesha.
“Miaka iliyopita, miezi kama hii tunakuwa bado tuna malighafi za kutosha na hata bei ya mafuta ilikuwa haipandi kamailivyojitokeza mwaka huu, na hii huwezi ukamlaumu mtu kwa sababu ni matatizo ya hali ya hewa ambayohayasababishwi na mtu,” amesema Mwakitalima.
Naye Samson Sangwe, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi kwenye moja ya viwanda hivyo, amesema kwa sasa hakuna biashara ya mafuta wala mashudu kutokana na kukosekana kwa malighafi.
Amesema wamiliki wa mashine hizo wanalazimika kuzifunga kwa sababu gharama za uendeshaji ni kubwa kuliko wanachopata, ameiomba serikali kukabiliana na tatizo hilo la uhaba wa mafuta.
Baadhi ya wafanyabiashara wa chakula maarufu mamalishe na baba lishe, wamesema kuadimika kwa mafuta nakupanda bei kumesababisha biashara zao kukwama kutokana na wengi wao kushindwa kumudu bei.