Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo nchini ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo huku ikisema ili kuleta tija katika uzalishaji wa mazao, Kilimo hutegemea teknolojia za Kilimo, utaalam na upatikanaji wa Pembejeo bora, ikiwemo mbolea.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge jijini Dodoma na kuongeza kuwa katika msimu wa kilimo 2022/2023, matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 538,000 sawa na ongezeko la asilimia 48.

“Ongezeko hili limetokana na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ambayo Serikali imekuwa ikitoa kuanzia msimu wa kilimo wa 2022/2023. ongezeko la matumizi ya mbolea limeenda sambamba na ongezeko la uzalishaji hususan mazao ya chakula ambapo upatikanaji wa chakula umeongezeka nchini,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Aidha, ameongeza kuwa makadirio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 ni tani 849,219 na kwamba hadi kufikia Agosti 31, 2023, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 480,662 sawa na asilimia 56.6 ya wastani wa mahitaji kwa mwaka.

Amesema, “katika msimu huu wa kilimo, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei ya pembejeo hii muhimu katika uzalishaji. Hivyo, ninaielekeza Wizara ya Kilimo kusimamia kikamilifu ugawaji wa mbolea kwa wakulima kwa kuboresha mfumo wa ugawaji ikiwemo kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea pamoja na kuvisogeza vituo hivyo karibu na wananchi.

Jorge Vilda: Nimegeuzwa mbuzi wa kafara
Diwani CCM achoshwa na mabadiliko