Denis Tililo (29), ambaye ni Mshauri wa kodi amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es salaam akikabiliwa na mashtaka nane likiwemo la utakatishaji fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mapato – TRA hasara ya Shilingi 118.9 milioni.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa serikali Theresia Mtao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rehema Lyana amesema Agosti 28, 2023 Buguruni Wilaya ya Ilala, mshtakiwa alitoa risiti ya uongo ya EFD kwa jina la Yasini Revelian kwa nia ya kumdanganya Kamishna Mkuu wa TRA ili kumlipa mfanyabiashara hewa Janeth Kitego VAT Shilingi milioni 7.6.
Aidha, mshtakiwa huyo pia anadaiwa kutoa risiti ya uongo yenye namba 342 kutoka kwenye mashine ya EFD kwa jina la Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishina Mkuu kumlipa Kitego VAT ya Sh milioni 30.5.
Mshauri huyo wa kodi anadaiwa kutoa risiti ya uongo namba 343 kutoka kwenye mashine hiyo iliyosajiliwa kwa jina la Revelian na kumdanganya Kamishina Mkuu kumlipa Kitego VAT ya Sh 27,457,627.12.
Wakili Mtao alidai Tililo alitoa risiti ya uongo ya namba 343 kupitia mashine hiyo ya EFD ya Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishna Mkuu kuwa anamlipa mfanyabiashara hewa ambaye ni Kitego mwenye TIN namba 143-472-604 Kodi ya Ongezeko la Thamani Sh milioni 27.4/-
Katika mashtaka mengine inadaiwa mshtakiwa alitoa risiti ya uongo namba 344 kwa kutumia mashine hiyo yenye kiasi cha Sh milioni 780 na kupotosha mfumo wa kodi wa TRA kwa lengo la kumdanganya Kamishina ili kumlipa Kitego VAT ya Sh 118,983,050.85.
Imeendelea kudaiwa kuwa ikinyume na sheria na kwa makusudi aliisababishia TRA hasara ya Sh. milioni 118.9 kwa kutoa risiti za uongo ambazo zilikuwa zinalenga kutoa taarifa za uongo kwa Kamishina pamoja na mfumo wa mamlaka hiyo.
Katika shtaka la utakatishaji fedha, Tililo anadaiwa kufanya miamala ya fedha ya Sh. 118,983,050.85 wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa la uhalifu la kutumia risiti zisizo halali.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kikodi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo, wameiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Lyana ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kumtaka mshitakiwa kurudi rumande kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba moja ya shtaka linalomkabili la utakatishaji halina dhamana.