Tunalifungua kundi jipya leo, kundi E lenye mbabe Brazil akiwa na wakali wengine Switzerland (Uswiz), Costa Rica na Serbia. Kundi hili ni moja kati ya kundi ambalo michezo yake itaangaliwa kwa jicho la tatu na mabilioni ya watazamaji duniani kote.

Brazil imefuzu fainali za kombe la dunia ikitokea ukanda wa Amerika ya Kusini wenye mataifa ya Colombia, Chile, Paraguay, Peru, Argentina, Ecuador, Venezuela, Bolivia, Peru na Uruguay.

Brazil ilimaliza michezo ya kundi la ukanda huo kwa kufikisha alama 41 ambazo ziliwaweka kwenye nafasi ya kwanza.

Katika michezo 18 ya kundi hilo, Brazil ilishinda michezo 12, kutoa sare michezo 5 na walipoteza mchezo mmoja. Hivyo ilifuzu moja kwa moja katika fainali za 2018.

Majina ya utani ya timu ya taifa ya Brazil: Canarinho (Little Canary), Verde-Amarela (The Green and Yellow), Seleção (The Squad)

Mfumo: Kikosi cha Brazil hutumia mfumo wa 4-1-4-1.

Image result for Neymar - brazilMchezaji Nyota na nahodha: Neymar (Paris St-Germain)

Image result for Paulinho - brazilMchezaji hatari: Paulinho (Barcelona).

Image result for Adenor Leonardo Bacchi Tite - brazilKocha: Adenor Leonardo Bacchi Tite (56), raia wa Brazil.

Ushiriki: Brazil imeshiriki fainali za kombe la dunia mara ishirini (20). Mwaka 1930, 1934, 1938, 1950, 1954, 1958, 1962, 1966,1970, 1974, 1978, 1982, 1986, 1990, 1994, 1998, 2002, 2006, 2010 na 2014. Hii ni mara ya ishirini na moja (21).

Mafanikio: Kutwaa ubingwa (1958, 1962, 1970, 1994 na 2002).

Kuelekea 2018:

Brazil ni mabingwa wa kihistoria katika fainali za kombe la dunia tangu zilipoanzishwa mwaka 1930. Wanakwenda nchini Urusi wakiwa wanapewa nafasi kubwa ya kufanya maajabu makubwa, baada ya kushindwa kuzuia ubingwa usiondoke katika ardhi ya nyumbani kwao mwaka 2014.

Ujerumani waliowachabanga mabao saba kwa moja hatua ya nusu fainali, walizima ndoto za Brazil kuzuia kombe la ubingwa kuondoka nchini kwao, hivyo uwepo wa mabingwa hao watetezi, nao unachagiza morari kwa taifa hilo la Kusini mwa Amerika.

Kocha Tite anaamini mfumo wa 4-1-4-1 ambao ulimuwezesha kushinda michezo 20 tangu alipokabidhiwa kikosi cha Brazil mwaka 2016, utakuwa chachu kufikia malengo aliojiwekea.

Uwepo wa washambuliaji kama Neymar (PSG) na Gabriel Jesus (Man City) nao unampa ujasiri mkubwa, hasa baada ya wachezaji hao kuziwezesha klabu zao kutwaa ubingwa wa Ufaransa na England (Uingereza).

Pamoja na kufanikiwa kulipa kisasi cha kuifunga Ujerumani bao moja kwa sifuri katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki mwezi uliopita, bado mashabiki wengi duniani wanahitaji kuona kama kweli Brazil wamejidhatiti kuchukua ubingwa wa dunia kwa mara ya sita.

Wengine wanaomba timu hizo zikutane katika fainali za mwaka huu, ili kuthibitisha upinzani uliojengeka baina yao, hasa baada ya mabingwa wa dunia Ujerumani kuwafumua Brazil mabao saba kwa moja katika ardhi ya nyumbani kwao mwaka 2014.

Kikubwa ni kusubiri na kuona kama maombi ya mashabiki wengi wa soka duniani yataweza kujibiwa na Mwenyezi Mungu kwa namna wanayovyotamani iwe.

Brazil wataanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Switzerland (Uswiz), Uwanja wa Rostov mjini Rostov-on-Don Juni 17, kisha watapambana na Costa Rica Juni 22, Uwanja wa Krestovsky mjini Saint Petersburg, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Serbia Juni 27, Uwanja Otkritie mjini Moscow.

Brazil wanapewa nafasi ya kuweka ushindani mkubwa au hata kuwa kati ya timu nne zitakazoingia nusu fainali na hata fainali kwa kuzingatia historia. Hata hivyo, Brazil wanayochangamoto kubwa kwani vikosi vya timu nyingine pia vina hamasa nzito ya kuandika historia mpya.

Neymar, amethibitisha kuwa hakuna kitakachomzuia kushiriki kikamilifu mashindano ya fainali za kombe la dunia, majeraha aliyokuwa nayo yamepona kwa asilimia 100 na sasa yuko tayari kubeba ndoto ya Brazil nchini Urusi.

Je, watalibeba kombe ugenini kuponya donda walilolipata la kupoteza wakiwa nyumbani? Endelea kuwa hapa, tutakupeleka Urusi na yote yatafahamika kupitia Channel yetu ya Youtube ambayo ni Dar24 Media.

Kujipima ukimwi nyumbani kwazua sura mpya
Hatua 10 za kumlinda mwanao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kingono