Tunisia, moja kati ya mataifa ya Afrika yanayotinga nchini Urusi kusaka nafasi ya kuweka historia ya kunyakua Kombe la Dunia mwaka huu, ingawa historia yake hairidhishi sana.
Imepangwa Kundi G ikiwa na Ubelgiji, Panama na Uingereza.
Tunisia ni moja ya mataifa matano kutoka Afrika (CAF), yaliyofuzu katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu, ilipambana vikali kwa lengo la kurejea kwenye fainali hizo baada ya kuzikosa kwa miaka 12 iliyopita.
Timu ya taifa ya Tunisia ilipangwa kundi A (Kundi La Kwanza) lililokuwa na timu za mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya na Guinea.
Michezo ya kundi hilo ilikuwa sita, na Tunisia walifanikiwa kushinda minne, wakitoka sare miwili na hawakupoteza mchezo, hatua ambayo iliwawezesha kufikisha alama 14 ambazo ziliwapa nafasi ya kuongoza msimamo wa kundi hilo.
Kwa mafanikio hayo Tunisia ilikata tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia 2018 moja kwa moja.
Majina ya utani ya timu ya taifa ya Tunisia: Los Canaleros (The Canal Men) na La Marea Roja (The Red Tide).
Mfumo: Kikosi cha Tunisia hutumia mfumo wa 4-2-3-1.
Mchezaji Nyota: Youssef Msakni (Al-Duhail)
Mchezaji hatari: Naïm Sliti (Dijon, akitolewa kwa mkopo kutoka Lille)
Nahodha: Aymen Mathlouthi (Al-Batin)
Kocha: Nabil Maâloul (55), raia wa Tunisia.
Ushiriki: Tunisia imeshiriki fainali za kombe la dunia mara nne (4). Mwaka 1978, 1998, 2002, na 2006.
Mwaka 1978 ambapo fainali hizo zilifanyika nchini Argentina, iliandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kushinda mechi ya kombe la dunia, ikiipiga Mexico 3-1.
Kuelekea 2018:
Taifa la Tunisia lenye watu zaidi ya 11,304,482 linafuzu fainali za kombe la dunia mwaka huu, baada ya miaka 12 kushuhudia wakikosa kushiriki kutokana na kushindwa kufikia lengo la kupambana, na kupata nafasi kutoka ukanda wa bara la Afrika (CAF).
Shirikisho la soka nchini humo lililazimika kumfukuza kazi kocha kutoka nchini Poland Henryk Wojciech Kasperczak mwaka 2017, baada ya kikosi chake kupoteza mchezo wa robo fainali wa fainali za Afrika.
Kocha mzawa, Nabil Maâloul aliteuliwa kukiongoza kikosi cha Tunisia mwezi Aprili mwaka 2017 na alikabidhiwa jukumu la kuhakikisha Tunisia inafuzu kucheza fainali za kombe la dunia.
Kocha huyo mzawa kwa kutumia mfumo wa 4-2-3-1, kila kikosi chake kilipoingia kucheza mchezo wa kuwania kufuzu, alifanikiwa kufikia lengo la kuivusha Tunisia katika mazonge ya kutoshiriki fainali za kombe la dunia kwa kipindi kirefu.
Mbinu za kumtumia beki wa upande wa kushoto Ali Maâloul (Al Ahly) kama sehemu ya mashambulizi ya timu ya Tunisia, ni moja ya mafaniko yaliyoonekana kufikiwa na kocha Nabil Maâloul.
Matumizi ya viungo mashuhuri na shupavu Ferjani Sassi na Mohamed Amine Ben Amor, nayo yalichagiza mafaniko yaliyopatikana wakati wa kusaka safari ya kuelekea Urusi.
Wachezaji wengine walioongeza chachu ya mafanikio hayo ni Youssef Msakni, Wahbi Khazri, Naïm Sliti na Ghailene Chaalali.
Tunisia wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Uingereza (England), Uwanja wa Volgograd mjini Volgograd Juni 18, kisha watapambana na Ubelgiji Juni 23, Uwanja wa Otkritie mjini Moscow, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Panama Juni 28, Mordovia mjini Saransk.
Zimebaki siku tatu tu kushuhudia mchezo wa kwanza wa fainali hizo na Dar24 inakusogeza Urusi kilaini. Kaa nasi hapa, mwambie na rafiki. Kesho tutamulika timu nyingine katika kundi hili na kumaliza na kundi la mwisho kabla ya kipyenga cha mitanange ya FIFA.