Ni hatua kwa hatua tunaendelea kuisogelea Juni 15 kushuhudia mtanange wa kukata na shoka, Dar24 inaendelea kumulika timu moja baada ya nyingine, leo tunaendelea na kundi E tukiigusa Uswisi.
Uswisi imeweka kwenye chungu cha kundi E pamoja na Brazil, Costa Rica na Serbia.
Timu ya Taifa ya Uswisi ilifuzu fainali za kombe la dunia 2018, ikitokea ukanda wa barani Ulaya (UEFA), ilipokuwa imepangwa katika kundi B (Kundi La Pili) lililokuwa na timu za Ureno, Hungary, Visiwa vya Faroe, Latvia na Andora.
Uswisi ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo kwa kufikisha alama 27, sawa na Ureno waliokuwa vinara, lakini walizidiwa kwa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo taifa hilo lenye watu zaidi ya 8,401,120, lililazimika kusubiri mchezo wa hatua ya mtoano ili kujihakikishia kucheza fainali za mwaka huu.
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kushirikiana na lile la barani Ulaya (UEFA) liliipanga Uswisi na timu ya taifa ya Ireland ya Kaskazini kucheza mchezo wa mtoano.
Mchezo wa mkondo wa kwanza kwa timu hizo ulichezwa Novemba 09, 2017 mjini Belfast katika uwanja wa Windsor Park, na Uswisi walifanikiwa kuwachapa wenyeji bao moja kwa sifuri lililofungwa na beki wa kushoto Ricardo Iván Rodríguez.
Mchezo wa mkondo wa pili ukachezwa Novemba 12, 2017 mjini Basel katika uwanja wa St Jacob Park na timu hizo zilitoka suluhu, na moja kwa moja wenyeji Uswizi walikata tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia.
Majina ya utani ya timu ya taifa ya Uswisi: Schweizer Nati (Swiss Nati), La Nati (The Nati), Rossocrociati (Swiss national team) na literally Red (Crusaders)
Mfumo: Kikosi cha Uswisi hutumia mfumo wa 4-5-1.
Mchezaji Nyota: Granit Xhaka (Arsenal)
Mchezaji hatari: Denis Zakaria (Borussia Mönchengladbach).
Nahodha: Stephan Lichtsteiner (Juventus)
Kocha: Vladimir Petković (54), raia wa Bosnian-Herzegovinian.
Ushiriki: Uswisi imeshiriki fainali za kombe la dunia mara tisa (9). Mwaka 1934, 1950, 1954, 1962, 1966, 1994, 2006, 2010 na 2014.
Mafanikio: Kufika Robo Fainali (1934, 1938 na 1954).
Kuelekea 2018:
Mashabiki wa soka nchini Uswisi tayari wameshajipa matumaini makubwa ya kuona timu yao ikifika mbali katika fainali za mwaka huu, na wengine wanatamba kupitia mitandao ya kijamii kwa kueleza watachukua ubingwa wa dunia katika ardhi ya Urusi.
Kocha Vladimir Petkovic ameeleza nia yake ya kutaka kuvunja rekodi ya kuivusha Uswisi katika hatua ya robo fainali, na na kisha kuongeza nguvu na kuiweka kileleni.
Aliwahi kuzungumza katika mkutano na waandishi wa habari, “timu yangu ina wachezaji wazuri na wenye kutambua umuhimu wa kuitumikia, wanajua nini kinachotakiwa katika Taifa lao, ninaamini tutavuka na kuvunja rekodi ya kuishia hatua ya robo fainali.”
Kiungo Granit Xhaka anaaminiwa sana na kocha huyo katika mipango aliojipangia, kutokana na kuwa na msimu mzuri akiwa na klabu ya Arsenal ya Uingereza, japo klabu hiyo ilimaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi.
Wachezaji wengine kama Xherdan Shaqiri (Stoke City) na Steven Zuber (Hoffenheim), Stephan Lichtsteiner (Juventus), Ricardo Rodríguez (AC Milan), Fabian Lukas Schär (Deportivo La Coruña) na chipukizi Manuel Obafemi Akanji (Borussia Dortmund), pia ni tegemeo kubwa kwa kocha huyo.
Uswisi wataanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Brazil, Uwanja wa Rostov mjini Rostov-on-Don Juni 17, kisha watapambana na Serbia Juni 22, Uwanja wa Kaliningrad mjini Kaliningrad, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Costa Rica Juni 27, Uwanja wa Nizhny Novgorod mjini Nizhny Novgorod.
Kesho tutakuwa hapa tena kuimulika timu nyingine, hakikisha hauko mbali na Dar24 ili usiwe mbali na Urusi mwaka huu.