Urusi na Belarus zimeanza mazoezi makubwa ya pamoja ya kijeshi, ambayo yamepewa jina Zapad-2017, ambayo yamezitia wasiwasi nchi jirani na wanachama wa shirika la kujihami la nchi za Magharibi la Nato.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Urusi imesema kuwa wanajeshi 12,700 wanashiriki mazoezi hayo, lakini wataalamu wa Nato wamesema kuwa idadi inaweza ikawa iko juu zaidi ya hiyo.
Aidha Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko ameonya kuwa Zapad-2017 jina ambalo maana yake kwa Kirusi ni “Magharibi” huenda ikawa ni hatua ya mwisho kabla ya kuivamia Ukraine.
Hata hivyo, Makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi tayari wanayashikilia maeneo makubwa ya mashariki mwa Ukraine na wameendelea kukabiliana na wanajeshi wa nchi hiyo.