Mwanadiplomasia mkuu wa Urusi, Sergey Lavrov yupo katika ziara ya nchi nne za Afrika za Misri, Ethiopia, Uganda na Jamhuri ya Kongo wiki hii, akizilaumu nchi za Magharibi kwa uhaba wa nafaka unaohusiana na vita, uliozua hofu ya njaa.
Ziara ya Lavrov, inafuatia maendeleo ya mzozo unaozidi kukua ambapo Ijumaa Julai 22, 2022 Urusi ilikubali makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, ambayo yangeruhusu Ukraine kuuza nje nafaka yake.
Lakini, saa chache baadaye makombora ya Urusi yalishambulia mji wa bandari wa Odesa nchini Ukraine, kituo muhimu cha mauzo ya nje, chini ya siku moja baada ya mkataba huo kutiwa saini.
Hata hivyo, Serikali nyingi barani Afrika na Mashariki ya Kati zimekuwa zikijiepusha na mzozo huo, zikitaka kudumisha ufikiaji wa usafirishaji wa Urusi, licha ya shinikizo kutoka kwa Magharibi.
Katika hatua nyingine, shirika la Human Rights Watch limesema vikosi vya Urusi vimewatesa na kuwapiga raia katika maeneo ya kusini mwa Ukraine ambayo wanayadhibiti, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa dhuluma ambazo zinaweza kuwa uhalifu wa kivita.