Wakati Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans ikihusishwa kuwa mbioni kuinasa saini ya Makabi Lilepo awe mbadala wa Fiston Mayele, makocha wa zamani wa klabu hiyo wametofautiana na usajili huo huku wengine wakidai kuwa Mshambuliaji huyo hatoshi.
Taarifa zinaeleza kuwa, Young Africans imewaweka katika rada washambuliaji mbalimbali akiwemo Lilepo kuchukua nafasi ya Mayele anayetarajiwa kutimkia Pyramids ya Misri.
Lilepo raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), alionyesha kiwango kikubwa katika kikosi cha Al Hilal Omdurman ya Sudan msimu uliopita na kufanikiwa kufunga mabao manne katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na mabao saba aliyofunga Mayele katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu uliopita na kutwaa kiatu hicho.
Pia, Mayele alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupachika mabao 17 na kuisaidia Young Africans kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Tetesi za ujio wa Lilepo na kuondoka kwa Mayele zimewagawa baadhi ya makocha wa Young Africans kutokana na sababu mbalimbali walizoziorodhesha.
Aliyekuwa Kocha wa timu hiyo, Kennedy Kennedy Mwaisabula, amesema anaamini nyota huyo anaweza kufanya vyema katika kikosi hicho kwani hata wakati Young Africans inamsajili Mayele hakuwa amefunga idadi kubwa ya mabao.
“Mayele amekuwa na sifa kubwa baada ya kutua Young Africans, lakini alipokuwa anasajiliwa hakuwa mchezaji ambaye amefunga magoli mengi, naamini atawasaidia kuziba pengo,” amesema.
Hata hivyo, Charles Mkwasa alisema timu hiyo inahitaji straika mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kufunga kuliko alionao Lilepo.
“Hawatakiwi kusajili kwa mihemko, inatakiwa kutulia na kujiridhisha kuwa mchezaji anaweza kuwasaidia kwani wao ni wakubwa na wanatakiwa kufanya vizuri zaidi msimu ujao,” amesema Mkwasa.
Wakati huo huo Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe alisema mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kutulia kwani wapo mbioni kutangaza nyota wote waliowasajili kwa msimu ujao.
Hadi sasa Young Africans imeshawatambulisha wachezaji watano ambao ni Gift Fred, Kouassi Yao, Maxi Mpia Nzengeli na wazawa Nickson Kibabage na Jonas Mkude.
Pamoja na hao tayari timu hiyo imeachana na Eric Johora, Abdalah Shaibu ‘Ninja’, Dickson Ambundo, Tusila Kisinda na Bernard Morrison.