Utafiti mpya uliofanywa hivi karibuni na kampuni ya Infotrak umeonesha kuwa endapo uchaguzi mkuu ungefanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili zilizopita hadi leo, mgombea wa kambi ya Upinzani ya National Super Alliance (NASA), Raila Odinga angepata ushindi mwembamba dhidi ya mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta.
Utafiti huo umeonesha kuwa Odinga anaongoza kwa asilimia moja tu dhidi ya Kenyatta, akipata asilimia 47 huku Kenyatta akiwa na asilimia 46. Kwa mujibu utafiti huo, asilimia sita ya Wakenya bado haijajua itamchagua nani.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 49 ya Wakenya wanaamini kuwa nchi haiendi vizuri wakimlaumu Rais Kenyatta kwa hali ngumu ya maisha, rushwa na ufisadi pamoja na ubovu wa miundombinu.
Aidha, asilimia 47 ya Wakenya wamesema wanaridhika na utendaji wa serikali ya Rais Kenyatta na kwamba nchi inaelekea katika njia nzuri.
Utafiti huo ulifanyika katika majimbo 100 ya uchaguzi kwenye wilaya 31 tofauti ambazo Jubilee na NASA wana nguvu sawa, hali iliyoonesha kufungana katika kigezo cha umaarufu.
Akisoma matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Julai 16 na Julai 20 mwaka huu, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Angela Ambitho alisema kuwa asilimia 6 ya Wakenya kutoka Mikoa ya Magharibi ambao hadi sasa hawajafanya maamuzi, ndio watakaoamua nani awe Rais mpya wa Kenya kama watapiga kura yao Agosti 8.
Nairobi imeonekana kuwa ngome ya Raila Odinga akikubalika kwa asilimia 46 dhidi ya Kenyatta anayekubalika kwa asilimia 39 katika jiji hilo.
Tafiti kadhaa za awali zilikuwa zikimpa nafasi ya ushindi Rais Uhuru Kenyatta. Kampuni ya IPSOS ilieleza kuwa Kenyatta angepata asilimia 47 ya kura zote na Odinga angepata asilimia 43 ya kura zote endapo uchaguzi ungefanyika mwishoni mwa mwezi huu.