Serikali kupitia shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),imeanza kufanya utafiti wa mafuta ya Petroli katika bonde la Eyasi Wembere.
kwamujibu wa taarifa iliyotolewa na TPDC, utafiti huo unahusisha uchoraji wa visima vitatu vifupi, vya utafiti vyenye urefu wa mita 300 kila kimoja.
Lengo likiwa ni kukusanya sampuli za miamba (cores) kutathmini uwezekano wa miamba hiyo kuhifadhi mafuta.
Imeelezwa kuwa mchakato huu ni baada ya kazi ya awali ya kukusanya taarifa kwa anga (AGG) iliyofanyika mwaka 2015/2016 na kuonesha uwepo wa miamba yenye kuweza kuhifadhi mafuta katika eneo hilo.
Hivyo basi mita 900 zitachorongwa katika bonde la Eyasi Wembere ambapo kisima namba moja kinachorongwa katika kijiji cha Kining’nila wilaya ya Igunga.
Visima viwili vinavyobaki vitachorongwa wilaya za Meatu mkoani Simiyu na Iramba mkoani Singida.
Eneo la Eyasi Wembere lipo katika bonde la ufa ambalo nchi jirani za Kenya na Uganda zimegundua mafuta katika mabonde yaloyopo kwenye bonde la ufa hivyo jiolojia ya Eyasi Wembere inafanana kabisa na ile ya Lokichar Kenya na Albertine Graben Uganda.