Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ambaye alikuwa amelazwa kwa siku tatu Hospitali mjini Roma kwa maradhi ya kupumua, ameruhusiwa baada ya hali yake kuimarika, huku akisema kwa kutania kuwa bado yuko hai.
Papa Fransis, alilazwa katika Hospitali ya Gemelli nchini Italia katikati ya wiki, akiwa na matatizo hayo ya kupumua, ambapo Wasemaji wa Vatican walikitoa taarifa kuwa atatoka hii leo Jumamosi April mosi, 2023 baada ya matokeo ya vipimo.
Papa huyo ambaye kwasasa ana umri wa miaka 86, amesema, “sikuwa na hofu, bado niko hai,” akiwaambia Waandishi wa Habari na Waombezi wa Heri nje ya Hospitali kabla ya kuruhusiwa kuondoka eneo hilo.
Hata hivyo, alionekana akiwa na nyuso ya tabasamu na kupunga mkono akiwa kwenye gari, kabla ya kutoka nje kuzungumza na umati. Kisha akaelekea makao makuu ya makazi yake Vatican.