Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imezitaka mamlaka za uteuzi katika ngazi mbalimbali ndani ya taasisi za umma na binafsi  kuzingatia usawa wa kijinsia katika kuhakikisha tunafanikisha dhamira ya kufikia uwakilishi wa nusu kwa nusu.

Waziri wa wizara  hiyo, Ummy Mwalimu ametoa wito huo jana kwa mamlaka za uteuzi ikiwa ni pamoja na wajumbe wa bodi mbalimbali za uongozi wa Idara na Taasisi, alipokuwa akizungumza na ujumbe wa wanaharakati wa maendeleo ya jinsia na watoto waliomtembelea ofisini kwake.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema kuwa serikali iko  katika mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria ya ndoa katika kifungu cha 13 na 17 ambacho kinarusu mtoto aliye chini ya umri wa miaka 17 kuolewa.

Alisema kuwa mabadiliko hayo yanafanyiwa kazi na kuahidi kuwasilisha muswada wake Bungeni kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Aidha, alisema kuwa ‘sheria ya elimu’ iliyopitishwa hivi karibuni Bungeni imewaacha bila ulinzi watoto wengi ambao hawako shuleni, hivyo ni jukumu la jamii nzima kuwalinda watoto hao wakati huu ambapo marekebisho ya sheria ya ndoa yanaandaliwa.

“Kwakuwa mabadiliko haya ya sheria ya elimu yaliyopitishwa na Bunge la 11 yawewaacha nje pasipo ulinzi wa sheria watoto wengi walio nje ya shule, kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi katika kuwalinda watoto hao,” anakaririwa..

Naye mkurugenzi wa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Liliani Liundi aliyeongoza ujumbe huo ofisini kwa Waziri ili kuwasilisha maoni yao juu ya changamoto zinazoikabili nchi katika kuleta usawa wa kijinsia, aliunga mkono wito uliotolewa na waziri na kuongeza kuwa kuna haja ya kuiangalia pia sheria inayozungumzia mirathi ili watoto wa kike wawe na haki ya kupata mirathi.

Hemed asimulia Maisha ya ‘uteja’ ya baba yake yalivyomfunza kuwa tofauti
Video: Mawaziri wa mambo ya nje Tanzania na Rwanda wakitiliana saini