Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko amesema Kampuni ya Uchimbaji madini ya dhahabu Geita (GGML) inaongoza Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kutekeleza kikamilifu mpango wa Uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), na kwamba Wizara inajipanga kutengeneza muongozo maalum utakaofanya utekelezaji wa miradi ya CSR bila kutegea.
Dk. Biteko ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea mgodi wa GGML ili kushuhudia miradi mipya ya uchimbaji wa dhahabu inayofanyika katika mgodi huo Mkoani Geita na kusema kwa muda mrefu GGML wamekuwa wakitekeleza kwa kiwango cha kuridhisha mpango wa CSR.
Amesema, “Mimi ningependa tuwe wa kweli, nchi hii kampuni inayofanya vizuri kwenye CSR kwenye madini ya kwanza ni GGM wamefanya kazi nzuri, GGML imekuwa ikishirikiana na wananchi katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii zinazozunguka migodi kama ujenzi wa hospitali, shule na vifaa vya tiba ili jamii ipate huduma bora.
Waziri Biteko ameongeza kuwa, ziara yake ililenga kuona hali ya mgodi baada ya kuhama kutoka kwenye uchimbaji wa shimo la wazi kwenda kwenye uchimbaji wa chini kwa chini na kusema “Hofu yetu ilikuwa ni juu ya mgodi huu kuwa kwenye hatua ya uendelezaji, tulidhani utashuka lakini sasa tunafurahi wamejitahidi kuweka uzalishaji kwenye kiwango kinachotakiwa.”
Kwa upande wake, Makamu Rais wa AngloGoldAshanti anayeshughulikia maendeleo kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri katika mazingira yote yanayozunguka mgodi na kumshukuru Dk. Biteko kwa kuipongeza GGML kwa ununuzi wa bidhaa na kutumia huduma za kitanzania.
Amesema, “Mtafahamu kwamba mgodi huu umekuwa wa uchimbaji wa wazi tangu kwa miaka 15, kuanzia mwaka 2002 hadi 2015… kuanzia mwaka 2015 tumeanza kuhamia chini kwa chini, kufikia leo tuna miradi mitatu mikubwa, mradi wa Star and commet, Nyankanga na Geita hill ambayo yote inazalisha na pia miradi hii inasaidiana na miradi ya wazi ya Nyamlilima.”
Shayo alisema, asilimia kubwa ya bidhaa za mgodi huo sasa karibu asilimia 70 ya fedha inayotumiwa na GGML inanunua bidhaa kutoka Tanzania, na kwamba lengo la GGML ni kuhakikisha inaendelea kuwa kinara kwa kufanya vizuri ili kuwavuta watu na ajira za Kampuni hiyo na wote wanaozunguka mgodi kuwa na ujirani wa manufaa.
Awali, Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM), aliipongeza GGML kwa kushirikisha kikamilisha wazawa wa Geita na watanzania kwa ujumla katika utoaji wa huduma mbalimbali ndani ya mgodi na kutoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotangazwa na GGML, ili kupata zabuni za kutoa huduma ndani ya mgodi huo.
Alisema, “Sisi Halmashauri ya Mji wa Geita ni wafaidika namba moja kwa sababu katika taarifa kwenye CSR inayotengwa tunapata asilimia 54 ya Sh bilioni tisa ambazo tumezielekeza kwenye maeneo manne makubwa ya elimu, miundombinu afya, miundombinu ya kawaida ya kijamii kama viwanja vya mpira, lakini sasa tunakwenda kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja, hakika tunaendelea vizuri.”