Eneo la maziko ya Rais, likifahamika kama Embassy Park jijini Lusaka, hapo ndipo alipolala Kiongozi mwenye historia katika Taifa la Zambia, Kenneth David Kaunda ambaye bila shaka alifariki akiwa ameridhika kwamba alishiriki ukombozi wa bara la Afrika kwa ushirikiano na Viongozi wengine akiwemo kinara wa mapambano, Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Kaunda alifariki Juni 17, 2021 akiwa na umri wa miaka 97 na kuzikwa Julai 7, 2021 kufuatia maombolezo ya kitaifa ya siku 21 yaliyotangazwa na Rais wa wakati huo Edgar Chagwa Lungu akiwa mwanzilishi pekee wa Umoja wa Afrika (AU), aliyesalia, wenzake wote walitangulia kabla yake.

Kimsingi, Siku ya Afrika inakusudiwa kuadhimisha kwa kutambua mafanikio ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU sasa AU) tangu kuundwa kwake Mei 25, 1963, katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi, pamoja na maendeleo ambayo Afrika inayoyahitaji, huku ikitafakari changamoto za pamoja ambazo inakabiliana nazo.

Hayati, Dkt. Kenneth Kaunda, (kulia) akijadili jambo na Robert Mugabe (kushoto) na Mwl. Julius K. Nyerere enzi za uhai wao katika majukumu ya uongozi (katikati) Picha na Mtandao.

Kwa kuwa, kifo cha Dkt. Kaunda kilipokelewa na majonzi mengi kutoka duniani kote, pamoja na wakuu kadhaa wa nchi za Afrika waliohudhuria mazishi yake, suala hili halikushangaza, kwani Kiongozi huyu alishiriki jukumu lake muhimu katika mapambano ya uhuru wa Afrika kutoka kwa utawala wa kikoloni.

Baada ya kupata uhuru Oktoba 24, 1964, na kujua kwamba Zambia ilijaliwa kuwa na maliasili nyingi kama vile madini na udongo wenye rutuba, Kaunda alikuwa huru kuchagua njia rahisi ya kusonga mbele dhidi ya tawala za ubaguzi wa rangi za Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe), Msumbiji, Afrika Kusini, Afrika Kusini Magharibi (Namibia), na Angola na kuwaweka Wazambia salama.

Dkt. Kaunda hata hivyo aliamua kuwa Zambia isingeweza kujiona kuwa huru wakati majirani zake wangali chini ya nira ya ukoloni na hivyo kutumia gharama kubwa za uchumi wa nchi, kuamua kuunga mkono harakati za uhuru kwa vyama vya ukombozi wa makazi kutoka kwa tawala za kibaguzi.

Robert Mugabe wa Zimbabwe (kushoto), akiwa na Kenneth Kaunda (katikati), enzi za uhai wao. Picha na Daily mail.

African National Congress (ANC), Afrika Kusini, FRELIMO – Msumbiji, South West Africa People’s Organization (SWAPO), Namibia, The Popular Movement for the Liberation of Angola (MPLA), na Union for the Total Independence of Angola (UNITA), Angola, Zimbabwe African National Union (ZANU) na Zimbabwe African People’s Union (ZAPU), zikiwa ni miongoni mwao.

Serikali ya Dkt. Kaunda, ikaanzisha kile ilichokiita Kituo cha Ukombozi cha Afrika katika Kitongoji cha Kamwala, Lusaka, ambako harakati hizi zote za ukombozi ziliendeshwa na ndipo tawala za kikoloni katika eneo hilo zilijibu kwa kuiteka Zambia kwa vitendo mbalimbali vya uchokozi, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kiuchumi, kwa nia ya kutaka kuwasilisha, lakini Dkt. Kaunda hakukubali.

Mwenyekiti wa SADC wakati huo, na Rais wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi, katika ibada ya kumbukumbu ya Rais, alisema kutokana na uungaji mkono wa Dkt. Kaunda kwa harakati za ukombozi, Zambia ililipa gharama kubwa kwa kuwa ilihujumiwa na utawala wa Rhodesia. na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, na kusababisha hasara ya maisha na uharibifu wa uchumi wake.

Viongozi wazalendo barani Afrika, Rais wa kwanza wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandela (kuhsoto), akiwa na Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda (katikati). Picha na VOA.

Nyusi alisema, uhuru wa Zambia chini ya Dkt. Kaunda mwaka wa 1964 ulikuwa msukumo kwa nchi nyingine za Kusini mwa Afrika akikumbuka kwamba makubaliano ya uhuru wa Msumbiji yalipitishwa Lusaka na Dkt. Kaunda kati ya FRELIMO na wakoloni wa Ureno mwaka 1974, na baadaye kufanikiwa kupata uhuru mwaka 1975.

Kaunda alionyesha kwamba, kufanya kazi kwa ajili ya watu hakumaliziki wakati muhula wa urais unapomalizika kwani aliutumia muda wake kupigania vita dhidi ya VVU na UKIMWI, na alihusika katika kazi mbalimbali za hisani baada ya kustaafu urais wa Zambia mwaka 1994.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, alieleza kwa usahihi kifo cha Kaunda kama ishara ya mwisho wa enzi ya wanafalsafa wakubwa wa Kiafrika na wapigania ukombozi akiwataja pia Dkt. Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta wa Kenya, Sekou Toure wa Guinea, Leopold Senghor wa Senegal na alama ya Bara la Afrika, Kiongozi muasisi wa Taifa la Tanzania, Julius K. Nyerere.

Kenneth Kaunda, akisalimiana na Fidel Castro wa Cuba. Picha na Rafael Perez wa AFP.

Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi wakati huo yeye alitoa pongezi kwa Kaunda kwa kuiingiza nchi yake katika OAU, kama mtangulizi wa AU na alisema uhuru wa Botswana haukuwa msukumo rahisi kutokana na nafasi ya utawala wa wazungu wachache nchini Afrika Kusini na kwamba, yote yaliangukia kwenye mabega ya Dkt. Kaunda kuwa kipaza sauti cha waBotswana.

Alimshukuru Dkt. Kaunda kwa kujenga urafiki kati ya Rais mwanzilishi wa Botswana, Sir Seretse Khama na Rais mwanzilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius K. Nyerere waliosababisha kuundwa kwa Nchi za Mstari wa Mbele kitu ambacho kama Kaunda angekuwa hai, basi angekataa kupata sifa zote kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa Afrika.

Lkini angekataa vipi wakati Julai 18, 2009, alipewa Tuzo ya Mafanikio ya Maisha kutambua mchango wake wa mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika na hasa Afrika Kusini na Zimbabwe, ambapo katika Banda la Sandton International Convention Centre, Johannesburg, aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akiwa na binti zake walimkabidhi Kaunda Tuzo hiyo, kwa niaba ya Jumuiya ya Urithi wa Afrika.

Kenneth Kaunda na Dk Martin Luther King, Jr. mwaka 1960 nchini Marekani (Picha na BBC)

Zaidi ya wageni 500 waalikwa, akiwemo Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu wa zamani wa Swaziland, Prince Dhlamini na viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa ANC wakiongozwa na mweka hazina mkuu wa chama hicho, Mathews Phosa, walihudhuria hafla hiyo kwa pamoja na Meya wa zamani wa Lusaka, Fisho Mwale na aliyekuwa mwenyekiti na mtendaji mkuu wa Bherens Limited, Abel Mkandawire.

Na kisha Kamishna Mkuu wa Zambia nchini Afrika Kusini, Leslie Mbula, ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumza katika hafla hiyo, alisema kuwa Zambia inajivunia kwamba, Jumuiya ya African Heritage Society imeamua kumkabidhi Kaunda Tuzo ya Mafanikio ya Maisha kwa kutambua mchango wake katika mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika.

Alibainisha kuwa, ni jambo la kawaida kwamba Zambia ilifanya kazi kwa ukaribu na vyama vya ukombozi kusini mwa Afrika, vikiwemo ANC ya Afrika Kusini, ZANU na ZAPU ya Zimbabwe, SWAPO ya Namibia, FRELIMO ya Msumbiji na MPLA ya Angola kwa msaada wa Tanzania chini ya Julius K. Nyerere.

Kenneth Kaunda aisalimiana na Yoweri Kaguta Museveni. Picha na The Independent Uganda.

Alisema, “Japo hili halikuenda vizuri kwa serikali ya Ureno ya kifashisti, kutokana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na utawala wa Ian Smith nchini Zimbabwe ambao waliitikia kwa kulipua miundombinu ya Zambia, katika kipindi ambacho Wazambia wengi walipoteza maisha yao.

Mbula anasema, Lengo la shambulio hilo, lilikuwa ni kutaka serikali ya Zambia itolewe na “Kampeni za ulipuaji wa mabomu, hata hivyo hazikufikia malengo yaliyokusudiwa, hasa kutokana na uthabiti wa serikali ya Zambia na watu wake na Zambia iliweza kukabiliana na tawala hizi za uhasama na kandamizi na haikukubali vitisho.

Kaunda alisisitiza tangu mwanzo kwamba, hakuna njia Zambia inaweza kujiona kuwa huru wakati majirani zake bado walikuwa chini ya ukoloni na kwa ajili hiyo, Zambia iliendelea kuunga mkono mapambano ya ukombozi hadi Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na baadaye Afrika Kusini ilipokombolewa kwa msaada mkubwa pia wa Mwl. Nyerere na baadaye Kaunda alishukuru kwa tuzo hiyo na kusisitiza heshima hiyo haiwezi kuhusishwa na kazi ya mtu mmoja.

Kenneth Kaunda na Joachim Chissano katika picha ya pamoja, Januari 11, 2006 Picha kwa hisani.

Alisema “Ni jumla ya michango ya watu wengi, ambao baadhi yao wanaweza kukosa fursa ya kutambuliwa, inatosha kusema kwamba mchango wao hauna thamani ndogo kwa sababu ulitoa kiungo muhimu cha kutimiza malengo yetu ya pamoja na ninafahamu kabisa kwamba watu wengi wameniwezesha kuheshimiwa kwa namna hii ya ajabu.”

Kaunda aliendelea kusema, “Mchango wao ni muhimu vile vile na kutambuliwa kwa mchango wa mtu kwa jambo linalostahili kunapaswa kutoa msukumo wa kufanya vizuri zaidi na ninaamini kwamba inapaswa pia kutoa hali ya kuridhika kwa wale wengine ambao walifanikisha kupitia juhudi zao za kujitolea.”

Dkt. Keneth Kaunda anakuwa ni moja ya alama za mashujaa wa kusini mwa Afrika ambao bila uoga aliweza kuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa nchi yake bila kuwasahau majirani wanaoizunguka Zambia na kuhakikisha kwamba kwa ushirikiano wanakuwa huru na kujiendesha wenyewe.

Keneth Kunda akisalimiana na mgeni wake Malkia Elizabeth II wa Uingereza wakati alipowasili nchini humo Julai 29, 1979. Picha kwa hisani.

Ukimtoa Kaunda, pia wapo viongozi wengi ambao wanastahili kuigwa kwa mazuri waliyoyafanya enzi za uhai wao ambayo yalikuwa nni kwa maslahi ya umma, na zaidi watabaki kukumbukwa kutokana na uletaji wa tunu za taifa katika nchi wanazotoka akiwemo Nelson Mandela, Kwame Nkurumah, Milton Obote na hapa kwetu Tanzania ni Julius Kambarage Nyerere ambaye mwezi huu tunaingia kufanya kumbukizi ya kitaifa ya Nyerere Day ambayo hufanyika Oktoba 14, kila mwaka.

Kumbukizi za Mwalimu Nyerere, zitaendelea kukuijia kupitia ukurasa huu wa Dar24 ili kutambua kazi za wapigania uhuru wa Taifa la Tanzani,a na jinsi Mwalimu alivyoshiriki katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika na wazo lake la kutaka Afrika iwemo moja, ikiwemo fikra zake na baadhi ya mambo ambayo bado yanaishi na yataendelea kuishi vizazi na vizazi wakati huu ambapo tunaendelea kumkumbuka.

Imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya Habari, Mashirina na kumbukumbu za watu Mashuhuri barani Afrika.

Twende na kasi ya Rais utengaji maeneo uwekezaji: Dkt. Mabula
AU yalaani mapinduzi Burkina Faso, EU yatoa tamko