Nchini India Mahakama ya juu imeamua kufutilia mbali kosa la uzinzi kuwa si kosa la uhalifu tena nchini humo katika hatua ambayo imefutilia mbali sheria ya kikoloni iliyodumu miaka 158.
Katika uamuzi wake mahakama hiyo imesema sheria hiyo imekuwa ikiwakandamiza wanawake na kuwafanya kana kwamba wao ni mali ya wanaume.
Kabla ya uamuzi huo mwanamume yeyote aliyeshiriki tendo la ndoa na mwanamke aliyeolewa bila idhini ya mume wake alikuwa ametenda kosa la uhalifu.
Mlalamishi aliyewasilisha kesi mahakamani, kupinga sheria hiyo alisema kuwa ni sheria ya kiholela na ambayo inawabagua wanaume na wanawake.
Haijabainika ni wanaume wangapi wameshitakiwa chini ya sheria hiyo kwa sababu hakuna taarifa zozote kuhusiana na suala hilo.
Hii ni sheria ya pili ya kikoloni kufutiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi nchini India mwezi huu.
Akitoa hukumu hiyo, jaji mkuu, Dipak Misra,amesema japo sheria hiyo inaweza kutumiwa kutatua masuala ya kijamii kama vile kuachana kwa mume na mke lakini, “haiwezi kuwa kosa la uhalifu”.
Taarifa hiyo imetolewa na chombo cha habari cha BBC Swahili.