Aliyewahi kuwa Meneja wa Klabu ya Manchester United, FC Bayern Munich na Ajax Amsterdam Aloysius Paulus Maria “Louis” van Gaal, amemkingia kifua meneja wa sasa wa FC Barcelona Ronald Koeman na kiungo Frenkie de Jong akidai kuwa wageni mara zote huwa wanalaumiwa klabu ikiwa na matatizo.
FC Barcelona imekua na wakati mgumu tangu ilipoanza kuwa chini ya Komen kuanzia msimu uliopita, na msimu huu 2021/22 umekua mgumu kwake katika michezo ya Ligi Kuu ya Hispania hadi Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
Van Gaal ambaye pia aliwahi kupita FC Barcelona kama Mkuu wa Benchi la Ufundi, amesema hashangazwi kuona Koeman naye atakabiliwa na wakati mgumu huko Camp Nou.
Na kiungo De Jong ametetea hali ya klabu hiyo hivi karibuni akisema kwamba, msimu bado ni mrefu na kwamba timu hiyo hiyo inaweza kufanya vizuri.
“Kila kitu kinakwenda sawa, na kuna mchango mkubwa kutoka kwa Frenkie kwani amekuwa na kiwango bora kabisa,” alisema akinukuliwa na Sky Sport.
“Lakini mambo yakiwa mabaya, watu wanaangaalia wageni. Na katika hili kocha pia ni mgeni na ni Mlohanzi.
“Nina uzoefu na hilo. Historia inajirudia. Lakini nafikiri Frenkie anafanya vizuri pamoja na Ronald na Memphis (Depay). Sidhani kama kuna tatizo kubwa.” amesema Van Gaal ambaye aliwahi kutwaa ubingwa mara mbili wa LaLiga, Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na UEFA Super akiwa na FC Barcelona kuanzia mwaka 1997–2000.
Licha ya wasiwasi wa Van Gaal kuhusu lawama anazoendelea kutupiwa Komen, Rais wa FC Barcelona Joan Laporta, ameamua kumbakiza meneja huyo kutoka nchini Uholanzi.