Waziri wa Elimu nchini Ufaransa, Gabriel Attal amesema wanafunzi katika shule za Serikali watapigwa marufuku kuvaa abaya, vazi ambalo linavaliwa na baadhi ya wanawake wa kiislamu baada ya sheria hiyo kuanza kutumika mara tu mwaka mpya wa shule unaoanza Septemba hatua ambayo imeibua mjadala miongoni mwa jamii.
Hatua hiyo inajiri baada ya miezi kadhaa ya mjadala kuhusu uvaaji wa abaya katika shule za Ufaransa, huku vyama vya mrengo wa kulia vikishinikiza kupigwa marufuku huku wale wa kushoto wakielezea wasiwasi wao kuhusu haki za wanawake na wasichana wa Kiislamu.
Mnamo 2010, Ufaransa ilipiga marufuku uvaaji wa nguo za kufunika uso hadharani jambo lililosababisha hasira katika jamii ya Waislamu milioni tano wa Ufaransa.
Ufaransa imekuwa ikipiga marufuku vikali mambo ya kidini katika shule na majengo ya Serikali, ikisema zinakiuka sheria za kilimwengu na kuvaa hijabu kumepigwa marufuku tangu mwaka 2004 katika shule zinazomilikiwa na serikali.