Utata mkubwa umeibuka katika bandari ya Dar es salaam mara baada ya vichwa viwili kati ya kumi na tatu vilivyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania TRL kuvikana na kusema kuwa halivitambui.
Aidha,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato (TRA) kutoa taarifa ya ununuzi wa vichwa hivyo vya treni vilivyoagizwa nje ya nchi.
Utata huo unatokana na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kununua vichwa hivyo kupitia mkataba wake na Kampuni ya FMD ya Marekani na kutengenezwa na Kampuni ya DCD ya Afrika ya Kusini
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi, Deusdedit Kakoko amesema kuwa vichwa hivyo vina nembo ya TRL na kwamba ulitokea mgogoro kati ya Shirika hilo na Kampuni iliyotengeza vichwa hivyo baada ya kugundua kuwa mchakato wake wa manunuzi haukuwa sahihi.
“Mradi huu wa ununuzi wa vichwa 13 vya treni ni sehemu tu ya mpango kabambe wa Serikali wa kuifufua na kuiimarisha TRL, chini ya mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN),”amesema Kakoko.