Kiungo kutoka nchini Nigeria na klabu ya Simba Victor Akpan amefunguka na kueleza namna alivyojiandaa na Presha kutoka kwa Mashabiki wa klabu hiyo, ambayo ina kiu ya kurejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania Bara na kufanya vyema Kimataifa.

Akpan alisajiliwa Simba SC miezi miwili iliyopita akitokea Coastal Union ya Tanga, na hadi sasa amecheza michezo kadhaa ya Kirafiki, huku akitemwa kwenye vikosi vilivyocheza michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar.

Kiungo huyo amesema wakati akisajiliwa Simba SC, alifahamu anakwenda kwenye Klabu yenye Presha kubwa ya kusaka mafanikio, huku Mashabiki wakihitaji kuona kiwango kizuri kwa kila mchezaji aliyesajiliwa, hasa baada ya timu yao kushindwa kufikia lengo msimu uliopita 2021/22.

“Nimeliweka hilo katika akili yangu tangu najiunga na Simba kuwa kutakuwa na presha kubwa, ila naamini nikipata nafasi ya kucheza nitafanya zaidi ya kile ambacho benchi la ufundi litakuwa likitegemea kutoka kwangu,”

“Simba kuna wachezaji wengi bora – waliokuwepo msimu uliopita nasi wapya. Natambua kutakuwa na ushindani mkubwa kuwania kucheza katika kila nafasi.

“Nataka kutoa mchango wa kutosha kwa timu ili kufanya vizuri katika mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika ili kupata mafanikio tofauti na msimu uliopita.

“Mara zote naamini mchezaji mzuri lazima atakutana na changamoto. Kwenye nafasi ambayo nacheza kuna Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni na Sadio Kanoute ila ikitokea nimepata nafasi nitajitahidi kuonyesha kiwango bora.” amesema Akpan

Mwishoni mwa juma lililopita Akpan alihusishwa na tetesi za kutaka kutolewa kwa Mkopo kwenye klabu yake ya zamani Costal Union, kufuatia kushindwa kuingia kwenye mfumo wa Kocha Zoran Maki, lakini hadi sasa Uongozi wa Simba SC haujasema lolote kuhusu tetezi hizo.

Mogadishu: Uokoaji wakamilika, vifo vyafikia watu 21
DC Kisarawe ahimiza ushirikiano zoezi la Sensa