Mshambuliaji Kimataifa wa Nigeria, Victor Osimhen amepanga kuishtaki klabu yake ya SSC Napoli kutokana na video ya dhihaka iliyowekwa kupitia akaunti yao ya Tik Tok inayomhusu yeye.
Nyota huyo ambaye aliisaidia klabu hiyo ya mjini Naples kubeba ubingwa wa Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 msimu uliopita, klabu yake ilimfanyia kebehi na kuzua gumzo mtandaoni.
Video hiyo ya Osimhen ilitengenezwa kutokana na kukosa Penati wakati wa mechi ya Serie A dhidi ya Bologna iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Hata hivyo, ni nadra sana kwa Mshambuliaji huyo kukosa Penati ambaye alifunga mabao 62 katika mechi 107 alizocheza Serie A, lakini video hiyo ya kumdhihaki ilimuonyesha Osimhen akimuomba refa awape Penati kwa kutumia sauti ya kushangaza.
Wakala wa Mshambuliaji huyo, Roberto Calenda, amethibitisha wazi kwamba Osimhen anataka kuchukulia hatua dhidi ya SSC Napoli kuhusu video hiyo ambao ilifutwa baadae.
Calenda ameandika kupitia akaunti ya X: “Kilichotokea kwenye akaunti ya Tik Tok ya Napoli hakikubaliki. Ukweli ni kwamba imemuathiri mchezaji, wamemuongezea matatizo kwani bado ana mgogoro na waandishi wa habari kuhusu taarifa feki kuhusu yeye. Tunataka haki ifuate mkondo wake.”
SSC Napoli haijatoa tamko kuhusu video hiyo huku kukiwa na bifu la chini chini kati ya Osimhen na kocha wake Rudi Garcia.