Mshambuliaji kutoka Nigeria na klabu ya SSC Napoli Victor Osimhen anajiandaa na mpango wa kutimkia Ligi Kuu ya England mwishoni mwa msimu huu.
Klabu ya SSC Napoli inaripotiwa kutambua mpango huo, hivyo imeanza kujiandaa kumsaka mrithi wa Mshambuliaji huyo, huku ikimtupia jicho Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Tammy Abraham.
Lakini, kwenye usajili wa Abraham, anayekipiga AS Roma kwa sasa, SSC Napoli watakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa timu nyingine.
Osimhen mwenye umri wa miaka 24, amefunga mabao 26 akiwa katika msimu bora kabisa huko SSC Napoli.
Na sasa Mnigeria huyo ameisogeza Napoli kwenye taji la Serie A wakibakiza alama chache tu kunyakua taji hilo.
Mtandao wa Tuttomercatoweb umedai kwamba Osimhen anajiandaa kuachana na klabu hiyo ya Italia na kutimkia England kama kutakuwa na ofa ya maana kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Chelsea inaelezwa kufukuzia saini ya Osimhen na huenda hilo likafanyika kwa nguvu zote itakapomchukua kochaMauricio Pochettino.
Manchester United nao wanamhitaji Osimhen aje kukipiga kwenye Ligi Kuu England.
Klabu nyingine kubwa za Ulaya zinazomtaka Osimhen ni FC Bayern Munich na Paris Saint-Germain. Lakini, mshambuliaji huyo mipango yake ni kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England.
Napoli wao wakimpoteza Osimhen watakwenda kumsajili Abraham, ambaye Mwingereza huyo amefunga mabao 35 tangu alipoachana na Chelsea kwenda Italia miaka miwili iliyopita.
Kutokana na kocha wa AS Roma, Jose Mourinho hatima ya maisha yake kutoeleweka vyema, jambo hilo linaweza kumsukuma Abraham kutimka.