Prof. Luoga amesema hayo leo Novemba 20, 2018 kufuatia operesheni ya kushtukiza ya kukagua maduka ya ubadilishaji fedha na baadhi ya maduka bubu ambayo hayana leseni lakini yamekuwa yakiendesha biashara kinyume na sheria.
“Uchunguzi wa Benki Kuu umebaini kuongezeka biashara ya ubadilishaji na utakatishaji fedha. Kuna maduka hayajasajiliwa lakini yanafanya biashara hii kinyume cha utaratibu,” amesema Profesa Luoga.
Profesa Luaga amesema ambao leseni zao zina makosa wanatakiwa kuzirejesha Benki Kuu kwani tayari zimefutwa na wanaoendesha maduka bila leseni kuacha mara moja.
“Wote watakaobainika kukiuka sheria watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na wote waliokuwa wanaendesha maduka hayo bila kufuata utaratibu leseni zao zimesitishwa,” alisema.
Prof. Luaga amesema kuwa opresheni hiyo ilihitaji ushiriki wa maafisa wengi sana kutoka vyombo mbali mbali vya usalama ili kuhakikisha kila mahali ambapo opereshini inaendelea kunakuwa na usalama wa kutosha.
Aidha, ameeleza kuwa operesheni hiyo ni ya tatu kufanyika ikiratibiwa na kitengo cha uchunguzi cha benki hiyo ambapo uchunguzi huo unafanywa kipindi ambacho BoT imesitisha maombi ya kuanzisha maduka mapya ya kubadilisha fedha.