Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa uchaguzi mdogo wa marudio unaotarajiwa kufanyika Septemba 16, 2018 umekuwa uchaguzi wenye mtihani kwao, kwa madai ya kukiukwa kwa baadhi ya sheria za uchaguzi ya mwaka 1985 na wapinzani wao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Katibu wa Itikadi wa Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole ambapo amesema kuwa wapinzani wao wamekuwa wakitumia lugha zisizo na staha pamoja na utoaji wa rushwa kwenye mikutano ya kampeni unaofanywa na baadhi ya viongozi wake.
“Wenzetu hawakutaka kuheshimu sheria za vyama vingi, hawakufata maadili ya uchaguzi wenzetu wameyapuuza yote kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985, niwaambie tu TAKUKURU, chama cha CHADEMA wanagawa fedha na sukari kule Monduli na tunalifahamu hilo, tunaomba lifuatiliwe,” amesema Polepole
Aidha, Uchaguzi wa majimbo ya Monduli na Ukonga unarudiwa kutokana waliokuwa wabunge wake kwa tiketi ya CHADEMA, Julius Kalanga kwa upande wa Monduli na Mwita Waitara kwa upande wa Ukonga kujiuzulu huku wakiwania tena nafasi hiyo kupitia CCM.
Hata hivyo, katika chaguzi hizo Tume ya Uchaguzi ilitangaza marudio ya uchaguzi katika kata 20 pamoja na majimbo matatu ikiwemo jimbo la Korogwe vijijini ambalo mgombea wake Timotheo Mzava wa CCM alipita bila kupingwa na pia katika kata chaguzi za kata 20 chama hicho kilipita bila kupingwa kwa kata 12.