Kampuni ya DataVision International iliyoko jijini Dar es Salaam inaandaa mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itakayowezesha simu za wanafunzi kutumika kama kompyuta za kujifunzia badala ya kuwazuia kuingia nazo shuleni.
Akizungumza na Dar24, mtaalam wa mifumo ya TEHAMA wa kampuni hiyo, Profesa Fred Mtenzi amesema kuwa kampuni hiyo itaanzisha mfumo ambao utawezesha kudhibiti matumizi ya simu za wanafunzi wawapo eneo la shule ili ziweze kutumika kama vifaa vya kujifunzia na sio vinginevyo.
Prof. Mtenzi amesema kuwa hatua hiyo imetokana na utafiti walioufanya kuhusu namna ya kutumia teknolojia kusaidia jitihada za Serikali kuboresha huduma ya elimu mashuleni.
“Kwahiyo badala ya kuzuia watoto kwamba wasipige simu, tunaweza kubadilisha hili na hizi simu zikatumika kama kifaa cha kujifunzia na zinaweza kufikia sehemu zikachukua nafasi kabisa ya kompyuta zinazotumika,” Prof. Mtenzi aliiambia Dar24.
“Ukienda kwenye shule nyingi za msingi na sekondari wanasema kwamba ‘hatuna kompyuta’, lakini simu ambazo ziko kila mahali ambazo zingetumika sasa kama kifaa cha kufundishia zinazuiwa kabisa,” aliongeza.
Alisema DataVision itatoa mifumo itakayofungwa kwenye shule husika ili simu zote za wanafunzi zinazoingia ziwe zinadhibitiwa na kutumika kama vifaa vya kujifunzia kwa kuzuia matumizi ambayo hayakukusudiwa kielimu.