Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, Kisare Makori amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na watendaji wa Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania, TACIP kwa kuweza kuwafikia wasanii katika maeneo yao ili kuwasajili na kuhakikisha wanapata mafanikio katika sanaa zao.
DC Kisare ametoa pongezi hizo katika Semina iliyowashirikisha Watendaji wa Kata na Mitaa ya Manispaa ya Ubungo kuhusu mradi wa TACIP ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Semina hiyo.
Ambapo amewataka watendaji hao kuhakikisha zoezi la usajili wa wasanii (TACIP-Mtaa kwa Mtaa) katika Wilaya ya Ubungo linatekelezeka vizuri kwa kutoa ushirikiano wa kutosha wa watendaji wa TACIP pindi watakapokuwa wakiendelea na shughuli hiyo.
Pia DC Kisare amewahimiza Wasanii wa Sanaa za Ufundi wanaoishi na kufanyia kazi katika Wilaya hiyo kujisajili katika mradi wa TACIP, ambao unaanza kuorodhesha wasanii kwenye Kata na Mitaa ya Ubungo Machi 18, 2019.
Aidha, ameipongeza Kampuni ya DataVision International ambayo imebobea katika masuala teknolojia, kwa kujikita katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbali mbali na kufanya ubunifu wa mifumo mbali mbali Serikalini na katika Taasisi na Mashirika binafsi ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa DataVision kwa kushirikiana na Shirikisho la Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania, TAFCA wanafanya kazi nzuri ya kuwaunganisha wasanii na kuwawezesha kupata huduma mbali mbali za msingi, kama uwezo wa kukopesheka, kupata bina za afya na hata urahisi wa kufanya kazi zao kwa kutambulika rasmi.
”Kwakweli wanachokifanya TAFCA na DataVision International ni kazi nzuri sana, wanamuunga mkono Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli katika kusaidia kuzalisha ajira kwa wananchi, hivyo nawapongeza sana kwa kazi hii nzuri,”amesema Kisare
Wajumbe wa TACIP waliohudhuria Semina hiyo ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamalle, Mkurugenzi wa Biashara na Uhusiano toka DataVision International, Teddy Qirtu na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasilano (TEHAMA) kutoka DataVision International, Dkt. Dkt. Shaban Kiwanga.
Ambapo kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema kuwa mradi huo ambao upo chini ya Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo inayoongozwa wa Waziri wake Dkt. Harrison Mwakyembe unalenga kuwafikia wasanii wote wa Sanaa za Ufundi nchini, ili kuwatambua na kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbali mbali katika kazi zao.
Naye Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamale akizungumza katika Semina hiyo, amesema kuwa kwa kutambua changamoto za wasanii hao, TACIP inaenda kuzitatua kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwasajili wasanii hao, kuwapa vitambulisho ambavyo vitawatambulisha popote watakapokuwa wanafanya kazi zao za sanaa, pia kupitia vitambulisho hivyo wataweza kukopesheka katika mabenki na kuongeza mitaji yao.
Zoezi la Usajili wa wasanii wa Sanaa za Ufundi Nchini (TACIP-Mtaa kwa Mtaa) linaanza katika Wilaya ya Ubungo baada ya kumalizika katika Wilaya ya Kinondoni, ambapo hivi karibuni ujumbe wa TACIP wamemtembelea Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ofisini kwake jijini Dar es salaam ili kumpa taarifa za maendeleo ya mradi huo ambao upo chini ya Wizara yake.
Waziri Mwakyembe amefurahishwa sana na maendeleo ya mradi huo kwani pamoja na changamoto mbali mbali zilizolipotiwa na wajumbe hao, lakini bado anaona lengo kubwa la kuwainua wasanii wa sanaa za ufundi nchini likifanikiwa kwa kiasi kikubwa kama ambavyo umekusudiwa na kuahidi ushirikiano wa karibu zaidi.
TACIP ni mradi wa utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania ambao umevumbuliwa na kampuni ya kizawa ya DataVision International iliyoko jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na masuala ya Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tafiti na Mafunzo, ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA) chini ya Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo. Mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.