Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ilala, Sophia Mjema amewahamasisha wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga katika Soko la Kariakoo akiwataka kuchangamkia fursa zinazoletwa na Mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
DC Mjema ametoa hamasa hiyo alipokuwa akishiriki kipindi cha ‘On The Bench’ cha Dar24, kipindi kinachowakutanisha viongozi na wananchi katika maskani moja na kujadili changamoto zinazowakabili na kuzitafutia utatuzi.
Mkutano wa 39 wa SADC unafanyika jijini Dar es Salaam ambapo leo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea maonesho ya nne ya SADC na kushuhudia bidhaa mbalimbali za Watanzania zilizowasilishwa.
Aidha, kama ilivyo lengo la kipindi hicho, Mkuu huyo wa Wilaya alisikiliza kero na changamoto za wafanyabiashara hao na kuzitatua, huku akiwasihi kuzingatia matumizi bora zaidi ya vitambulisho vilivyotolewa na Rais John Magufuli kwa ajili ya wajasiriamali wadogo.
Aliwataka kutoa taarifa za wale ambao hawana vitambulisho hivyo huku wakificha na kufanya biashara kati yao, wakitumia kitambulisho kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja.
Aidha, aliwataka wafanye biashara bila kuingilia miundombinu ya mabasi ya mwendo kasi au mashine za Serikali kwani Rais John Magufuli hakumaanisha kuwa wafanye biashara katika maeneo yoyote bila kuzingatia miundombinu hiyo.
Katika hatua nyingine, DC Mjema aliagiza kukamatwa kwa mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Philip, aliyelalamikiwa na mfanyabiashara mmoja mwanamke kuwa alimuuzia eneo na kisha kuendelea kumnyanyasa, kinyume cha sheria na taratibu kwani maeneo hayo hayauzwi.
Angalia video hii kuona kipindi cha On The Bench ambapo DC Mjema alikunywa kahawa na wamachinga na kuzifanyia kazi changamoto walizozieleza: